Muhamed Khamis (UoI) -Zanzibar
BUNGE la Afrika Mashariki (EALA) linaloendalea na vikao visiwani hapa, limepokea muswada wa kuzuia matumizi ya vifaa vinavyotokana na plastiki na kusomwa kwa mara ya kwanza.
Akiwasilisha kwa mara ya kwanza muswada huo, mbunge kutoka Rwanda, Parricia Hajabakiga alisema utekelezaji wa sheria hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti bidhaa za plastiki ambazo huharibu mazingira.
Alisema lengo la kubana na kuzuia matumizi yote ya vifaa vya plastiki zikiwamo taka za viwandani, hospitali, maeneo ya ujenzi na maeneo mbalimbali yanayoambatana na matumizi hayo.
Mbunge huyo alisema licha ya ongezeko la athari mbaya za mazingira zinazohatarisha afya za watumiaji wa bidhaa hizo, bado hali hiyo inaendelea kuongezeka siku hadi siku kutokana na bidhaa hizo.
Alisema bidhaa za plastiki athari zake ni kubwa katika mazingira na baadhi ya nchi zimeweza kudhibiti na hivyo kusaidia usafi na kudhibiti uharibifu wa mazingira.
Hajabakiga alisema muswada huo utaweka misingi imara ya kudhibiti mazingira kubaki salama kwa kuzuia kuzalisha bidhaa za plastiki ambazo zinaathiri vibaya mazingira hasa kwa kuzingatia bidhaa hizo huchafua hali ya hewa kutokana na moshi wake ingawa bidhaa zenyewe kwa mfano mifuko, huwa haziozi na hivyo kufanya ardhi iwe kavu.
“Lengo jengine la muswada huu ni kuwaleta karibu wanamazingira rafiki waweze kusimamia na kujua matumizi mbadala ya vifaa vilivyozalishwa kwa plastiki,” alisema.