24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Biteko: Kutotatua kero za wananchi kunamkera Rais

*Ataka Viongozi Serikalini kutatua kero za wananchi na si kusikiliza tu

*Aagiza viongozi kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti mashuleni kabla ya Machi

*Awasha umeme Kijiji cha Magodi na Kigandini wilayani Mkinga

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameeleza kuwa Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan anataka kuona viongozi wote wanatatua kero na changamoto za wananchi na kwamba anasikitishwa na baadhi ya viongozi ambao hawatatui changamoto za wananchi mpaka pale anapofanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko.

Dk. Biteko amesema hayo Januari 25, 2024 wakati akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Magodi na Kigandini wilayani Mkinga mkoani Tanga mara baada ya kuwasha umeme katika vijiji hivyo ambao umesambazwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Katika ziara yake kwenye Vijiji hivyo, aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba, Mbunge wa Mkinga ambaye ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

“Mhe. Rais anafanya kazi kubwa katika kila Sekta na mabilioni ya pesa yamekuwa yakipelekwa kila Mkoa kwa ajili ya kuboresha huduma za wananchi, nikitolea mfano hapa Tanga Serikali ya Awamu ya Sita imeshaleta shilingi Trilioni 2 na Bilioni 600 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kwenye umeme miradi inaongezeka kwani mmepata bilioni 133.6 huku Wilaya ya Mkinga ikipata bilioni Nane kwa ajili ya usambazaji umeme, Dkt. Samia anapambana ili kuwaletea maisha bora watanzania hivyo viongozi wengine tusiishie kusikiliza kero tu bali tuzitatue na kama kuna mahali tunahitaji watupe muda, tuwaambie kwa uwazi,” amesema Dk. Biteko.

Katika hatua nyigine, Dk. Biteko amewataka Wazazi na Walezi nchini kupeleka Shule watoto wote wanaostahili kuwa mashuleni katika kipindi hiki ambacho shule zimefunguliwa ili wapate elimu itakayowasaidia katika maisha yao na nchi kwa ujumla, akitolea mfano kwa Mkoa wa Tanga watoto walioripoti shule ni asilimia 60.

Hivyo, ameagiza viongozi kusimamia suala hilo ikiwemo kuendesha msako na kutumia sheria zilizopo kwa wale wanaoficha watoto ili wasiende shule kwani ifikapo mwezi Machi watoto wote wanatakiwa wawe wameripoti mashuleni.

Akizungumzia kuhusu usambazaji umeme vijijini, amepongeza REA kwa kuendelea kusambaza umeme vijijini akitolea mfano kuwa, usambazaji umeme vijijini mkoani Tanga umefanyika kwa asilimia 91 na wilaya ya Mkinga yenye Vijiji 85 tayari vijiji 82 vimesambaziwa umeme huku kazi ya kusambaza umeme kwenye vijiji vilivyosalia ikiendelea na baadaye vitafuata vitongoji.

Kuhusu hali ya umeme nchini, amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya kila jitihada kuboresha hali hiyo kwa kuhakikisha kuwa mitambo ya umeme inafanyiwa maboresho na miradi mipya inaanzishwa na kutekelezwa akitolea mfano kituo cha umeme cha New Pangani (MW 68) kinatarajiwa kuzalisha umeme baada ya siku mbili baada ya kufanyiwa maboresho.

Akiwa katika Kijiji cha Magodi, Dk. Biteko amechangia Sh milioni 5 kwa ajili ya kusaidia kubadilisha paa la zahanati ya kijiji hicho ambalo limechakaa na kuahidi kumalizia ujenzi wa jengo la Madrasa katika Kijiji hicho.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mkinga ambaye ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula ameishukuru Serikali kwa kutekeleza kwa ubora miradi ya umeme vijijini wilayani humo na kuwafanya wananchi kufanya shughuli za kiuchumi pamoja kuboresha utoaji wa huduma kwenye maeneo mbalimbali kama vile vituo vya Afya na Shule.

Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kusambaza umeme kwenye maeneo mengine yaliyosalia kama vile vitongojini ili wananchi katika maeneo hayo pia wapate huduma ya umeme.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles