22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Bilioni 120  zahitajika kutengeneza wahandisi mahiri

Winfrida Mtoi na Ester Mnyika

Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini(ERB), Mhandisi Bernard Kavishe, amesema  kiasi cha fedha Sh 120 bilioni kinahitajika  kwa mwaka ili kutengeneza wahandisi mahiri kupitia Mpango wa Mafunzo kwa Vitendo kwa  Wahandisi Wahitimu(SEAP).

Amesema hayo leo Februari 28, 2024 wakati wa kufunga  maadhimisho ya miaka 21 ya SEAP  na semina ya siku tatu  kwa wahandisi wahitimu jijini Dar es Salaam.

Amesema fedha hizo zitatumika kugharamia mahitaji kwa wahandisi wapya wahitimu 10,500 wa mafunzo ya vitendo  kupitia mradi huo.

“Kwa mwaka wahandisi wapya wanaomaliza vyuo Tanzania na wengine kutoka nje ni takribani 3500,  kwa sababu ni mpango wa miaka mitatu tunaongelea wahandisi takribani 10,500, wale kuwatunza kwa mwezi mmoja ni bilioni 10.

“Kwa maana hiyo mpango huu tungefanya kwa asilimia 100 usaidizi, ungetupeleka mbali kwenye kuongeza kiwango cha wahandisi na ingerudi tu kwa sababu hawa tungewarudisha kwa jamii na kuwapeleka site na wangefanya kazi kwa weledi.

“Kwa  hiyo tunaomba Serikali kupata chanzo endelevu cha kusaidia hawa vijana ili mpango wa SEAP usiwe wa hiari uwe wa lazima kama fani ya udaktari,”  ameeleza Mhandisi Kavishe.

Amefafanua kuwa uhitaji wa soko la wahandisi  mahiri nchini ni  12,000  ikiwa kama nchi ya uchumi wa kati, kwani mhandisi mmoja anatakiwa kuhudumia watu  kama 5000.

Naye mgeni rasmi katika hafla hiyo ya kufunga,  Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania, Dk. Gemma Modu amewataka wahitimu hao mafunzo waliyopewa katika semina hiyo.

Aidha ameishukuru Serikali ya Norway  iliyotoa ufadhili wa wahandisi wa kike na kuwataka wanufaika  kuhakikisha wanafuata maelekezo ili bodi iendelee kupata miradi mingine.

Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa mradi wa SEAP mwaka 2018-2021, Mhandisi Nancy Mduma ambaye ni Mhandiri Msaidizi Chuo cha Maji,  amesema ni mpango muhimu kwa wahandisi wahitimu wa chuo kwa sababu wanapitia mafunzo maalumu ya kitaaluma na kwenda kuwa wataalamu.

“Zaidi ya yote niwashukuru sana wale wadau wote walioweza kusapoti mpango huu wa SEAP, nawapongeza sana bodi kwa  kuwa nipo hivi nilivyo kwa sababu yao. Binafsi nimefaidika sana na mafunzo haya na moja ya faida ni ujuzi wa kitaaluma,” ameeleza Mhandisi Nancy.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles