Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Katika kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza majaribio ya treni ya mwendokasi inayotumia umeme kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kuelekea hatua ya kuanza rasmi ifikapo mwishoni mwa Julai.
Wakati akihutubia Taifa Desemba 31,2023 Rais Samia aliliekeleza TRC kuhakikisha linaanza rasmi safari za Dar es Salaam – Dodoma ifikapo Julai,2024.
Leo Aprili 21,2024 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amezindua majaribio ya treni hiyo ambapo safari hiyo imehusisha pia viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali kwa lengo la kuweka baraka katika usafiri huo.
“Hii ni moja kati ya shughuli iliyoko kwenye ratiba ya sherehe za Muungano kuzindua njia ya reli ikionyesha kuwa reli hii sasa imekamilika, hatua zilizobaki ni chache ili tuanze safari rasmi.
“Nchi yetu inathamini dini ndiyo maana tunaendelea kushirikiana na viongozi wa dini zote na kutoa uhuru kwa Watanzania kushiriki kwenye dini kulingana na imani zao.
“Tunaamini hatua tuliyofikia ya kuendeleza tunu za taifa hili inatokana pia na Watanzania kuwa na imani za kidini, Rais Samia aliona ni vema viongozi wa dini wasafiri wenyewe kwa reli hii, tunaweka historia ya aina yake, nyie ndiyo mnaiombea reli hii ianze kazi vizuri,” amesema Majaliwa.
Amesema taifa limejengewa misingi imara ya kuheshimu dini kwa kuwa ina mchango mkubwa kwenye maendeleo ya taifa na kwamba maendeleo hayawezi kupatikana kama hakuna amani.
“Tutaendelea kufungua milango ya mazungumzo kwa viongozi wa dini, kusikia ushauri wenu, kupokea yale yote mnayofikisha kwenye jamii yetu ili nchi iendelee kuwa na amani. Tanzania ni nchi iliyoteuliwa na Mungu kwa utulivu wake na amani na uvumilivu tulionao siri yake kubwa ni uwepo wa dini, uwepo wa viongozi wenye karama. Bado tuna matumaini makubwa nanyi kuifanya nchi hii kuwa na utulivu na serikali itaendelea kuwashirikisha katika matukio yote,” amesema.
Waziri Mkuu amesema viongozi wa dini wameirahisishia serikali kufanya kazi zake kwa urahisi kwa sababu wamechukua nafasi kubwa ya kuwasihi Watanzania kuwa watulivu na kusababisha Tanznaia kuwa kimbilio la nchi zilizokosa amani katika nchi zao.
Amesema Rais Samia ana dhamira ya kuhakikisha miradi yote ya kimkakati iliyoanzishwa awamu ya tano inaendelea kama vile ujenzi wa meli, viwanja vya ndege, ununuzi wa ndege, daraja la Busisi, Bwawa la Nyerere na kwamba wana uhakika kufikia mwaka 2025 watakuwa wamefikia hatua nzuri.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, amesema ujenzi wa reli hiyo umegawanywa katika vipande vitano ambapo cha Dar es Salaam – Morogoro kimefikia asilimia 98.93, Morogoro – Dodoma (asilimia 96.61), Makutupora – Singida – Tabora (asilimia 14.22), Tabora – Isaka na Isaka – Mwanza (asilimia 56.21).
“Majaribio yalianza kufanyika baada ya kupokea vichwa na vitendea kazi vingine ili kuhakikishja usalama na ufanisi wa vifaa ambavyo vitatumika kusafirisha mizigo na abiria,” amesema Kadogosa.
Kwa mujibu wa Kadogosa hadi kufikia Aprili,2024 wameshapokea mabehewa 65, seti moja ya treni ya kisasa inayotumia umeme (EMU) na vichwa tisa kati ya 17 vinavyotakiwa.
“Tuna treni za kutosha kubeba watu wa Dar es Salaam kwenda Dodoma, tuna uwezo wa kutoa treni kila baada ya saa moja. Tunaishukuru na kuipongeza serikali kwa kuendeleza ujenzi wa miundombinu hasa reli ya kisasa. Reli hii itachagiza mapinduzi ya sekta ya viwanda, kilimo, ujenzi, kilimo, ufugaji,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema watakaonufaika kwa haraka na reli hiyo ni wakazi wa mkoa huo kwani ni kiunganishi kikubwa na mikoa mingine.
“Haya ndiyo maendeleo ya watu, kila mmoja aendelee kuliombea taifa kuhakikisha usafiri huu unakuwa na tija kwa taifa letu,” amesema Chalamila.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema wanaendelea kutekeleza maagizo ya Rais Samia kuhakikisha ifikapo Julai huduma za usafiri huo zinaanza.