Na Ramadhan Hassan,Dodoma
MFUMUKO wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba mwaka 2020 umepungua hadi asilimia 3.0 kutoka asilimia 3.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba mwaka 2020.
Hayo yalielezwa leo Jumanne, Desemba 8, mwaka huu, jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Sensa ya watu na Takwimu za jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ruth Minja alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari.
Mkurugenzi huyo amesema hali hiyo inamaanisha kwamba kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba mwaka 2020 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba mwaka 2020.
Amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba 2020 kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula kwa kupindi kilichoishia mwezi Novemba 2019.
Mkurugenzi huyo amevitaja bidhaa hizo na asilimia kwenye mabano kuwa ni pamoja na mchele (4.5),mahindi (14.3),unga wa mahindi (5.7),unga wa mtama (4.4),viazi vitamu (2.6) vyakula vya watoto lishe (1.8) na ndizi za kupika (4.9).
Amesema kwa upande wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Novemba 2020 umepungua hadi asilimia 2.8 kutoka asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia mwezi oktoba 2020.