Godfrey Shauri -Dar Es Salaam
MGANGA wa kienyeji Omari Rashidi (64), mkazi wa Wazo Msikitini, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, amepandishwa kizimbani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kwa kosa la ulawiti.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Dorith Massawe, akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi John Chacha, alidai kati ya tarehe zisizojulikana mwaka 2018 na mwaka 2019, mtuhumiwa alimwingilia kinyume na maumbile mtoto wa miaka nane.
Mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri ukisema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe kwa kusomwa tena.
Katika hatua nyingine, Mkazi wa Madale, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Athumani Rajabu (28), amefikishwa katika mahakana hiyo akikabiliwa na shtaka la ubakaji.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Dorith, alidai mbele ya Hakimu Mwamini Kazema kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo eneo la Goba Kulungwa Desemba 28, mwaka jana.
Wakili Dorith alidai tarehe zisizojulikana mwaka jana na Desemba 28 mwaka huo huo, mtuhumiwa alimbaka mtoto mwenye umri wa miaka 12.
Hata hivyo mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na Dorith alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba terehe kwa kusomwa tena.
Hakimu Kazema alisema dhamana ipo wazi endapo mshtakiwa atakidhi vigezo vya kuwa na wadhamini wawili waaminifu watakaotoa Sh 500,000 kila mmoja na wenye barua kutoka taasisi inayotambulika au barua kutoka Serikali za Mitaa.
Mshtakiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana hivyo alirudishwa rumande hadi Machi 30.
Wakati huo huo, mkazi wa Goba Neenia Eliasi (20), amepandishwa kizimbani katika mahakama hiyo akikabiliwa na tuhuma ya ubakaji.
Awali akimsomea mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi Kazema, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Dorith alidai kati ya Julai 2019 na Januari 19 mwaka huu mshtakiwa alimbaka binti mwenye miaka 15.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo huku upande wa Jamhuri ukidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika.