LONDON, UINGEREZA
WABUNGE 344 wa Uingereza wamekataa mapendekezo ya makubaliano ya Brexit ya Waziri Mkuu, Theresa May, juzi kwa mara ya tatu na kuashiria uwezekano wa kujiondoa mapema katika Jumuiya ya Ulaya, ikiwa ni ishara ya kutimuliwa vumbi ambalo linamchafua waziri huyo na huenda ikamlazimu kuitisha uchaguzi mkuu wa tatu nchini humo katika kipindi chake.
Uamuzi wa kuukataa mpango uliofupishwa kidogo wa makubaliano ya kujitoa katika Jumuiya hiyo kati ya Waziri May na Umoja wa Ulaya imeliacha suala la kujitoa kutoka Umoja huo katika hali ya sintofahamu kwa sasa, lini na ama hata iwapo Uingereza itajitoa na kulitumbukiza suala hilo la mzozo wa Brexit lililodumu kwa muda wa miaka mitatu sasa katika kiwango kikubwa cha kutoeleweka linaelekea wapi.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail, Waziri Mkuu, Theresa May aliungwa mkono na wabunge 286, ambao hawakufua dafu mbele ya wenzao 344 ambao wamekataa mapendekezo ya Waziri Mkuu huyo, hivyo kulilazimu taifa hili kuharakisha mchakato wa kujiondoa kwenye Jumuiya ya Ulaya.
Nalo gazeti la Telegraphy limeripoti kuwa, kwa matokeo hayo pia yanaashiria kuwa Waziri May anapaswa kujiuzulu mara moja baada ya kufanya majadiliano ya muda ya kuongeza uanachama wa muda wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya kushindikana.
“Hapaswi kuona au kuambiwa, kwamba wakati anaweza kukutana na Umoja wa Ulaya kujadili kurefushwa kwa muda wa kujiondoa kwenye Jumuiya ya Ulaya, ni kitu cha kawaida kwamba ndio amefika mwisho. Ni lazima ajiondoe, kwa ajili ya Brexit, kwa chama chake na demokrasia yenyewe,” ilisema tahariri ya gazeti la Telegraphy.
Aidha, gazeti hilo linalopendelewa na wanachama wa chama cha May cha Conservative na kuunga mkono juhudi za chama hicho katika siasa za Uingereza.
Hata hivyo, uwezekano wa kuwa na Waziri Mkuu mpya kuongoza awamu ijayo ya majadiliano ya Brexit ilikuwa haitoshi kuweza kuwavutia wabunge wa nchi hiyo katika zoezi la upigaji kura, baadhi yao wakihofia makubaliano yake yanaiacha Uingereza ikifungwa katika Umoja wa Ulaya iwapo mazungumzo ya hapo baadaye ya biashara yatavunjika.
Vyombo vya habari nchini Uingereza vimechambua kura hiyo kama hatua ya kuelekea kung’olewa madarakani kwa Waziri Theresa May au kuitisha uchaguzi mwingine. May, ambaye amenusurika katika changamoto ya kumtoa madarakani Desemba mwaka jana, amedokeza bungeni hapo juzi kwamba angehitaji kuitisha uchaguzi mkuu wa taifa kuweza kupata wingi kwa ajili ya kupitisha sheria ya Brexit.
“Uwezekano wa May kuitisha uchaguzi na kuongoza kundi la wabunge wa chama chake cha Conservative kupata wabunge wengi watakaofikia theluthi ya wabunge wote bungeni, ni vigumu,” limesema gazeti moja.
Nchini Uingereza, vyombo vya habari vimepambwa na maoni ya kumtaka Theresa May kujiuzulu wadhifa wake kwakuwa ameshindwa kutafuta ufumbuzi wa Brexit.
Kwa upande wake, gazeti la Daily Mail ambalo linaunga mkono Brexit limeeleza uamuzi wa bunge kupiga kura dhidi ya mipango ya Theresa May kuwa ni ‘usaliti’.
Kutokana na kura hiyo, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk, ameitisha kikao cha baraza hilo ifikapo Aprili 10 mwaka huu, kujadili hali ya mambo ya mpango wa Uingereza kujitoa.
Viongozi kadhaa wa Ulaya wamesema kuna nafasi halisi kwamba Uingereza sasa itajiondoa bila kupata makubaliano ya kibiashara, hali ambayo makampuni yanahofia itasababisha mtafaruku kwa uchumi huo wa tano mkubwa duniani.