Na ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM
HATUA ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuikana kampeni ya kukabiliana na vitendo vya ushoga iliyoanzishwa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, imewaibua watu wa kada mbalimbali nchini.
Taarifa hiyo iliyotolewa juzi ilieleza kuwa anachokifanya Makonda ni msimamo na mawazo yake binafsi na siyo msimammo wa Serikali.
Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, wadau wamesema hatua hiyo imeonyesha umuhimu wa kuheshimu utawala wa sheria na kuwaelekeza viongozi kuacha tabia ya kutumia madaraka yao watakavyo.
Katika tamko na agizo lake, Makonda aliwataka wananchi kutaja majina ya watu wanaodhaniwa kuwa mashoga na kumfikishia kwa ujumbe wa simu waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Jana, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume alisema tamko la wizara ni funzo kwamba Serikali na watendaji wake wanatakiwa kuheshimu sheria za nchi na za mataifa kuhusu faragha za watu na hata kama kuna haja ya kuingilia ni vema kutekeleza mambo kwa kufuata sheria
Alisema hatua ya Makonda kutaka watu watangaze hadharani watu wanajihusisha na mapenzi ya jinsia moja si sahihi kwa kuwa wapo wengine wanachafuliwa majina yao na kuumizwa kutokana na chuki binafsi, huku kukiwa hakuna uthibitisho wowote wa utaalamu na hata wa mazingira.
Alisema athari ya hatua hiyo ni kubwa kwa watu ambao wanaweza kujikuta wakitajwa kwa chuki ili kuchafuliwa majina hasa kwa kuwashushia heshina na kuwaumiza kisaikolojia, suala ambalo haliwezi kufidiwa inapobainika kuwa walisingizwa.
“Kimsingi katika namna aliyokuwa akitoa maagizo yake, Mkuu wa Mkoa hakuwa sahihi kabisa hasa katika suala la kuwambia watu wataje majina ya watu wanaodhani wanajihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
“Anatakiwa atambue na kwa hatua ya wizara, iwe funzo kwake kwamba kuna utawala wa sheria na ni vema pia aheshimu sheria,” alisema Fatma
Alisema Tanzania siyo kisiwa na kwa kuwa inaishi kwenye jamii na jumuiya ya mataifa, imetia saini mikataba kadhaa ya kulinda na kuheshimu haki za raia wake, suala linalotakiwa kuheshimiwa na yeyote bila kujali nafasi yake katika uongozi.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria la Haki za Biunadamu (LHRC), Anna Henga alisema barua hiyo ya Serikali kueleza kuwa hatua ya Makonda ni utashi wake binafsi, ni sahihi na imetolewa wakati muafaka.
Alisema kila jambo linatakiwa kushughulikiwa kwa kujali na kuheshimu misingi ya sheria za nchi na haki za binadamu na si kutokana na mapenzi au fikra za mtu.
Henga alisema kwa sasa bado wanaendelea kufuatilia kwa karibu athari zinazotokana na agizo la mkuu huyo wa mkoa.
Alisema kwa kuwa bado kuna mitazamo tofauti kati ya wadau wa kutetea haki za binadamu, kituo hicho kitatoa tamko rasmi wakati wowote.
“Hadi sasa bado inaonekana kuna mitazamo tofauti kidogo baina ya wadau wa haki za binadamu kwa hiyo tumeamua kutolizungumzia suala hilo kwa sasa, hadi tutakapojiridhisha kuwa tuko katika nafasi nazuri ya kutoa tamko,” alisema.
Muda mfupi baada ya kutolewa taarifa hiyo ya Serikali juzi, katika akaunti yake ya Twitter, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na baadaye Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne, Balozi Khamis Kagasheki aliandika:
“Najaribu kujifunza kuhusu Serikali yangu. Tarehe 30 Oct. Makonda atangaza kusaka mashoga. Serikali ipo. Aunda kamati ya watu 15. Serikali ipo. Tarehe 31 Oct. atangaza kupokeamsgs 5,763 na majina 100 ya mashoga. Serikali ipo. Leo siku ya 6 Serikali yamkana lakini haijamzuia.”
Katika akaunti yake ya Twitter, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema: “Serikali imekiri kuwa matendo ya Rc Makonda juu ya homosexual siyo msimamo wake kwani inaheshimu Katiba/Mikataba ya Kimataifa juu ya haki za Binadamu.
“Kama Serikali ingeheshimu haki ya Katiba na utawala wa sheria kwa mambo ya msingi, ni dhahiri Tanzania ingekuwa ni mfano wa utawala bora.”
Katika ukurasa wake wa Twitter, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliandika juzi muda mfupi baada ya kutolea kwa barua ya Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, akisema:
“Kwenye hili hatutakata tamaa. Nia yetu ni njema. Elimu bora na maadili mema ndiyo msingi wa maendeleo ya mwanadamu.”
Andiko hilo lilitumwa muda mfupi baada ya kusambaa video iliyomuonyesha akiwa katika ibada kwenye Kanisa la Efatha, ambako aliangua kilio alipokuwa akimuomba kiongozi wa Kanisa hilo, Mtume na Nabii Josephat Mwingira kuliombea taifa na hasa jamii iwe yenye maadili yanayokubalika katika imani.
Katika ukurasa huo, mmoja wa wachangaji, Fahami Matsawili alimjibu Makonda akisema: “Nia yako ni njema ya kuokoa kizazi hiki na kijacho dhidi ya madawa ya kulevya, ushoga….Tupo pamoja kaka kila ulipoanzisha vita hii kuanzia ya kwanza ya madawa na ya sasa ya ushoga walijitokeza wengine kupinga, simamia kilichosahihi ukweli haujawahi kushindwa unaweza kuchelewa tu.”
Kampeni hiyo ilianza wiki mbili zilizopita na wiki iliyopita, Makonda alisema tayari ana majina zaidi ya 100 ya watu wanaodaiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja na alipata zaidi ya ujumbe 18,000 kupitia simu yake kutoka kwa watu wanaolaani ushoga.
Katika kuchukua hatua zaidi, wiki iliyopita Makonda alitangaza kuunda kamati maalumu ya watu 17 kuhakikisha watu wanaofanya biashara chafu ya ngono wanachukuliwa hatua za sheria.
Kamati hiyo ilijumuisha watu kutoka Bodi ya Filamu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), polisi kutoka kitengo cha kuzuia uhalifu wa mitandao, madaktari na wanasaikolojia.
Makonda alisema kamati hiyo itafanya kazi katika makundi manne.
Alisema itakuwapo kamati itakayoshughulika na mashoga wanaojitangaza na wasiojitangaza lakini wanajulikana, kamati itakayowashughulikia wote wanaotengeneza picha au video za ngono ambako mpaka sasa tayari ana uthibitisho wa taarifa za nyumba 24 ambazo zinashughulika na kazi hiyo.
Makonda alisema kamati nyingine itaangazia watu wote wanaotangaza biashara ya ngono kwa njia ya mtandao ya jamii kama instagram, whatsapp na facebook na kundi la mwisho ni kamati itakayoangalia kundi la watu wanaofanya utapeli kwa njia ya mtandao kwa kutumia majina ya watu wengine vibaya kujipatia fedha.
Aliagiza pia, kufikia jana, Jumatatu Novemba 5, kila mtu ahakikishe hana picha chafu ya ngono katika simu yake kwa sababu hatua hiyo itaanza rasmi siku hiyo.