25.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 31, 2023

Contact us: [email protected]

Nondo: Sitarudi nyuma kutetea wanyonge

FRANCIS  GODWIN Na RAYMOND  MINJA – IRINGA


SAA chache baada ya kuachiwa huru   na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo, ameeleza magumu aliyopitia wakati akitetea wanafunzi huku akiwa anaendelea na kesi yake ya kudaiwa kujiteka.

Hukumu hiyo ya kesi ya jinai namba 13 ya mwaka 2018 ilitolewa jana na  Hakimu Mfawidhi, Liad Chemshana wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa.

Katika kesi hiyo  ilidaiwa kwamba Machi 7 mwaka huu akiwa Ubungo Dar es Salaam, Nondo  alichapisha taarifa hizo akitumia simu ya kiganjani yenye No. 0659366125 kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao na kusambaza katika mitandao ya jamii.

KAULI NONDO

Akizungumza nje ya mahakama  baada ya hukumu hiyo, Nondo  alisema katika kipindi chote wakati anatetea haki za wanafunzi   na kuendelea na kesi dhidi yake, alipita kwenye nyakati nzito katika  maisha yake ila anamshukuru Mungu kwa vile  Mahakama imetenda haki.

Alisema pamoja na hali hiyo, kamwe hatorudi nyuma katika mapambano ya kutetea haki za wanafunzi nchini kwa kupaza sauti   mambo yanapopindishwa.

“Katika  kipindi  chote  ambacho  nilikuwa napitia mapito  haya  mazito  iwapo  ningekuwa sina  msimamo ningekuwa  nimerudi  nyuma na kukata  tamaa kukubali  kila  nilichoshinikizwa  niseme  niweze kuachiwa.

“…  lakini  sikuwa  tayari kwa hilo nilimtanguliza Mungu  ambaye leo (jana),  ameweza  kunipigania, namshukuru Mungu na Mahakama kwa kutenda haki.

“Pia naushukuru Mtandao wa  Watetezi wa  Haki za Binadamu (THRDC),  muda wote wamekuwa nami, asanteni sana mawakili wangu, asanteni Watanzania wote sitorudi nyuma kuwa mtetezi wa wanyonge,” alisema Nondo.

Alisema amepita  katika mapito mazito kwa ajili ya kupigania  haki za  wanafunzi na kamwe hataacha kuendeleza harakati za kupigania haki zao.

“Mungu ni mwema ametenda mema juu yangu na sitarudi nyuma, nawaombeni niwashukuru pia waandishi wa habari  nchini hasa Iringa ambao muda wote mlifika kufuatilia  kesi  yangu naomba leo (jana)  niishie hapa.

“Nitasema zaidi ila leo (jana) sipo vizuri nina furaha kubwa,” alisema Nondo huku akibubujikwa machozi

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo ole Ngurumwa, alisema  Mahakama imeweza kutenda haki na uamuzi uliotolewa na mahakama hauna hata chembe moja ya upendeleo .

Katika  kasi hiyo, Nondo alikuwa  akitetewa na mawakili   wawili, Chance Luoga na Jebra Kambole  ambao walieleza imani kubwa  kwa mahakama kupitia hukumu hiyo.

Wakili Kambole alisema kuna uonevu mkubwa ambao  polisi walionyesha kumtendea mteja wao ambao mahakama  pia  imeuona.

Hukumu  hiyo  ilichukua    saa moja  kusomwa  huku  askari  wa  Kikosi cha  Kutuliza  Ghasia  (FFU)  wakiwa  wametanda nje ya mahakama  hiyo.

MAHAKAMA ILIVYOHUKUMU

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Chemshana alisema kwa  mujibu wa ushahidi wa Nondo mahakamani hapo,  alitekwa  eneo la Ubungo   Dar es Salaam na  watekaji    wakiwa katika  gari walikuwa wakimhoji mshtakiwa  kuwa nani yupo nyuma ya maandamano yaliyokuwa  yamepangwa kufanyika ya kupinga mauaji ya mwanafunzi   Akwilina Akwilini wa Chuo chaUsafirishaji (NIT).

Alisema kutokana na  ushahidi  uliotolewa  na mshatakiwa pamoja na Jamhuri hapana shaka kuwa Nondo alikwenda  polisi kama mlalamikaji ila polisi walimchukua kama mtuhumiwa .

“Mahakama  hii imeptia ushahidi na majumuisho ya  kesi hii   na kujiridhisha  bila shaka  yoyote  kuwa makosa  mawili ni  kueleza  uongo na  kurusha  uongo mitandaoni  ni  jambo  lisilo na ubishani ila  ni nani  aliyeeleza taarifa  hizo na kurusha  uongo.

“Swali la kujiuliza,  je, jamhuri wameshindwa kueleza  kuwa mshtakiwa  alifikaje Mafinga?

“Pili Mahakama imekosa ushahidi kuhusu alifikaje Mafinga, tatu, hakuna ushahidi  kutoka Jamhuri kuwa mshatikiwa alikuwa wapi wakati wa tukio.

“Hivyo mashahidi wa Jamhuri wametoa ushahidi wa hisia,” alisema   Hakimu Chamshama

Hakimu  alisema  swali la nne ambalo halina majibu ni Jamhuri wameshindwa  kuthibitisha uongo wa mshatikiwa kwa kila  namna na hata kielelezo  kilicholetwa na Jamhuri kinatia shaka… kwa mkanganyiko huu mahakama imejizuia  kuyaamini maelezo  yaliyoletwa  mahakamani.

Alisema ujumbe uliotumwa kupitia simu ya Nondo  uliosomeka ‘Am at risk!’ kwa  maana nipo hatarini, haukueleza hatari ya nini na haujulikani  ulitumwa  na nani ambako upande wa Jamhuri ulishindwa kutolea  ushahidi .

Hakimu Chemshama alisema mtu aliyepelekwa kutoa ushahidi kama mpenzi wa Nondo alisema aliwasiliana na Nondo  ila hakusema Nondo yupi, wapi na ujumbe wa ‘Am At risk’ uliotumwa haukutumwa na mshtakiwa  ingawa ulitumwa kwenye kundi la WhatsApp.

Alisema ushahidi wa shahidi wa tatu kama  ulivyo hauonyeshi  ni maagizo kutoka kwa mshtakiwa .

Hakimu alisema  si jukumu la Mahakama kujua mshtakiwa alitekwa au hakutekwa, hilo ni jukumu la polisi hivyo mahakama imeamua Abdul Nondo aachiwe huru.

Aisema  asiyeridhika na hukumu hiyo ana haki ya kukata rufaa   mahakama ya juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,315FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles