VATICAN CITY,Vatican
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amewatangaza kuwa watakatifu, Askofu Mkuu aliyeuawa El Salvado, Óscar Romero na Papa John Paulo VI .
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Papa Fransis alimtangaza kiongozi huyo wa zamani jana katika ibada.
Alimsifia kwa kuwa balozi wa amani wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo na kujitoa sadaka kuwa karibu na maskini na watu wake.
Askofu Romero aliuawa mwaka 1980 na wanajeshi wakati akiendesha ibada na hadi sasa wauaji wake hawajawahi kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mbali na Askofu mkuu huyo, Papa Francis vilevile alimtangaza Papa Paul VI, kwa mchango alioufanya katika kuleta mabadiliko katika Kanisa Katoliki miaka ya 1960.
Mwandishi wa BBC nchini humo, Will Grant alisema hatua ya Askofu Romero kutangazwa kuwa mtakatifu imekuwa ikiombwa na na Wakatoliki wengi katika nchi hiyo.
“Sisi tunatangaza na kuwaelezea Papa Paulo VI na Óscar Arnulfo Romero Galdámez … kuwa watakatifu na tunawaandikisha kati ya watakatifu kwa sababu wanapaswa kuheshimiwa na kanisa lolote,” kiongozi mkuu huyo wa Katoliki aliuambia umati wa watu wapatao 60,000 walihohudhuria ibada hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Mtakatifu Petro.
Pia katika ibada hiyo kiongozi huyo aliwatangaza watu wengine watano kuwa wenye kheri akiwamo yatima aliyefariki duni kwa saratani ya mifupa na mtawa mmoja raia wa Ujerumani.
Maelfu ya mahujaji walijitokeza kutoa heshima kwa watakatifu hao wapya wakiwamo 5,000 raia wa El Salvado.
BBC ilieleza kuwa Askofu Romero alitangazwa kuwa mwenye kheri Mei 2015 katika ibada iliyofanyika El Salvador na kuhudhuriwa na maelfu ya waumini wa kanisa hilo.