Na IBRAHIM YASSIN-ALIYEKUWA RUKWA
KATIKA jitihada za kupambana na mimba za utotoni mkoani Rukwa, wenyeviti wa vijiji na viongozi wa kata wametakiwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wazazi na walezi wanaowaozesha watoto wao katika umri mdogo, hali inayosababisha washindwe kuendelea na masomo.
Hayo yalisemwa juzi na Mratibu wa Shirika la Kiwohede, Salim Mpanda, katika mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi hao wa Wilaya ya Kalambo, ambapo alisema ni lazima wazazi wahakikishe wanafuatilia myenendo ya watoto wao kama njia ya kuwaepusha na vishawishi vinavyosababisha mimba za utotoni.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Dankeni Kipeta, alisema kwa kutambua ongezeko la mimba za utotoni wilayani humo, wameanza kutoa elimu ya kuwajengea uwezo viongozi hao wa vijiji kama njia ya kutokomeza hali hiyo.
“Jamii nzima ina umuhimu wa kuwatunza watoto wa kike ili wapate elimu sawa kama ilivyo kwa wa kiume badala ya kuwaingiza kwenye vishawishi vya kushiriki ngono wakiwa kwenye umri mdogo,” alisema.
Awali akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kalambo, Frank Sichalwe, alisema Serikali imejipanga kuchukua hatua kwa watu wanaowatorosha wanafunzi, hali inayochangia wasimalize masomo yao.