MKAA WAANZA KUTAFUTIWA MBADALA WAKE

0
694

Na ASHURA KAZINJA-MOROGORO


SERIKALI imesema iko mbioni kuandaa mkakati maalumu utakaowafanya wananchi watumie nishati mbadala kupikia badala ya kutumia mkaa.

Chini ya mkakati huo, wananchi hao watalazimika kutumia gesi au mkaa unaotokana na pumba badala ya kutumia mkaa unaotokana na miti.

Hayo yalielezwa jana mjini hapa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Aloyce Nzuki, alipokuwa akifungua kikao cha wataalamu wa masuala yanayohusu usimamizi wa sekta ya misitu nchini.

“Asilimia 80 ya Watanzania wanatumia mkaa na inaonekana mkaa huo unatokana na ukataji ovyo wa miti. Mkaa huo unatumika zaidi katika maeneo ya mijini na ili kukabiliana na changamoto hiyo, vinahitajika viwanda vidogo vitakavyotengeneza mkaa kwa kutumia vumbi la mbao.

“Matumizi ya gesi nayo ni muhimu ndiyo maana Serikali inataka kuhakikisha viwanda vidogo vilivyopo vinatengeneza nishati mbadala ili matumizi ya mkaa wa miti yaweze kupungua,” alisema Dk. Nzuki.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dosantos Silayo, alisema idara ya misitu ina wajibu wa kulinda rasilimali za misitu ikiwamo kukutanisha wadau wa misitu na wananchi kama sera ya misitu ya mwaka 1,998 inavyotaka.

“Pamoja na hayo, kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya misitu ikwamo ushiriki mdogo wa wananchi katika uhifadhi wa misitu, changamoto ya ukusanyaji wa maduhuli na utaratibu wa mgawanyo wa mapato kwa wananchi na Serikali.

“Kwa hiyo, naamini baada ya mkutano huu ambapo wadau wanajadili mambo mbalimbali, watakuja na njia mbadala ya kuhakikisha changamoto zote zinazoikabili sekta ya misitu zinatatuliwa,” alisema Profesa Silayo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dk. Ezekiel Mwakalukwe, aliwataka washiriki wa mkutano huo kujadili kwa kina masuala ya sekta ya misitu ili ipatikane njia ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here