TAASISI ZAPAMBANA MIMBA ZA UTOTONI

0
529

Na IBRAHIM YASSIN-ALIYEKUWA RUKWA


KATIKA jitihada za kupambana na  mimba  za  utotoni  mkoani Rukwa, wenyeviti  wa vijiji na viongozi wa kata wametakiwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wazazi na walezi wanaowaozesha watoto wao katika umri mdogo, hali inayosababisha washindwe kuendelea na masomo.

Hayo yalisemwa juzi na Mratibu wa Shirika la Kiwohede, Salim Mpanda, katika mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi hao wa Wilaya ya Kalambo, ambapo alisema ni lazima wazazi wahakikishe wanafuatilia myenendo ya watoto wao kama njia ya kuwaepusha na vishawishi vinavyosababisha mimba za utotoni.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Dankeni  Kipeta,  alisema kwa  kutambua ongezeko la mimba  za utotoni  wilayani humo, wameanza kutoa elimu ya kuwajengea  uwezo  viongozi  hao wa vijiji kama njia ya kutokomeza hali hiyo.

“Jamii nzima ina umuhimu wa kuwatunza watoto wa kike ili wapate elimu sawa kama ilivyo kwa wa kiume badala ya kuwaingiza kwenye vishawishi vya kushiriki ngono wakiwa kwenye umri mdogo,” alisema.

Awali  akifungua  mafunzo  hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kalambo, Frank Sichalwe, alisema Serikali imejipanga  kuchukua  hatua kwa watu wanaowatorosha wanafunzi, hali inayochangia wasimalize masomo yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here