29.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

ROMA MKATOLIKI:TUMEPIGWA,KUTESWA

NORA DAMIAN Na ESTHER MNYIKA-DAR ES SALAAM


MSANII wa hip hop, Ibrahim Mussa maarufu Roma Mkatoliki, amesema wana hofu juu ya usalama wa maisha yao. 

Roma na wenzake watatu, walitekwa Jumatano iliyopita na watu wasiojulikana,kisha wakaonekana Jumamosi asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alikiri walitekwa na kwamba hadi sasa hajui sababu zilizosababisha yeye na wenzake kutekwa.

Roma ambaye aliambatana na wenzake waliotekwa, Emmanuel Mtunya (house boy), Monii Central Zone, Bin Laden na mkewe Nancy Daniel, alisema walipigwa mno na hadi sasa hali zao kiafya si nzuri.

“Tukio lililotokea ni la kweli kabisa, tumepigwa, tumeumia, hatuna uhakika na usalama wetu. Hatuwezi ‘kurisk’ maisha yetu kwa sababu ya fedha au kwa ‘interest’ za watu wengine.

“Siko sawa kiafya na hata wenzangu, mnaona mwili wangu (anafunua fulana na kuwaonyesha waandishi sehemu mbalimbali za mwili wake zenye majeraha).

“Kama alifanyiwa daktari, msanii usishtuke kesho akifanyiwa mwandishi wa habari au mwanasiasa,” alisema Roma.

JINSI WALIVYOTEKWA

Alisema Aprili 5, mwaka huu, saa 11 jioni alikwenda katika studio za Tongwe zilizoko Masaki Dar es Salaam ambapo alikutana na wenzake, wakiwa wamewasha kompyuta kwa ajili ya kusikiliza muziki, ghafla walivamiwa.

“Jumatano iliyopita kati ya saa 11 na 12 jioni, nilikwenda studio  niliwakuta wenzangu tukawa tunasikiliza muziki. Baada ya nusu saa walikuja watu wakiwa na silaha za moto na kutuambia tuingie ndani ya gari.

“Tulifungwa vitambaa usoni na pingu, kasha kupelekwa kusikojulikana, tulikuwa tukihojiwa huku tukipigwa, tumeumizwa,” alisema.

Alisema ilipofika Ijumaa usiku, waliondolewa  sehemu waliyokuwa na kuingizwa ndani ya gari, huku wakiwa wamefungwa vitambaa usoni na miguu na kupelekwa kusikojulikana  na  kuachwa kwenye dimbwi la maji.

“Baada ya kuachwa eneo lile, nilijifungua kitambaa usoni na kugundua ilikuwa ni usiku sana, pia niliwafungua wenzangu, kisha tukaanza kutembea. Kila gari iliyokuwa ikipita na kutumulika tulikuwa tunajificha pembeni kwanza hadi ipite alafu  tunaendelea na safari,” alisema.

Alisema walitembea hadi walipofika sehemu ya kuona kibao kimeandikwa ‘Mahaba Beach’ na kugundua kuwa eneo hilo ni Ununio.

“Tuliendelea kutembea hadi tukafika Kunduchi na pembeni tuliona pikipiki zimeegeshwa, kwa kuwa mimi nguo zangu zilikuwa zimetapakaa damu nilimuomba Monii aende kuzungumza na wale madereva ili waje watupakie mishikaki.

“Lakini alipokaribia alisikia redioni zikitangazwa taarifa za kutekwa kwetu hivyo tukaingiwa na hofu, tukajitahidi wale bodaboda wasitugundue, tukatembea mbele kidogo tukaona bodaboda nyingine tukakodi na kupanda mishikaki,” alisema.

Alisema walielekea nyumbani kwake Mbezi ambapo walikuta nyumba imefungwa aligonga mlango bila mafanikio na kuamua kuvunja mlango wa nyuma na kuingia ndani.

“Hata nilipovunja mlango na kuingia ndani sikukuta mtu, hali ile ilizidi kuniogopesha,ilikuwa inaelekea alfajiri. Niliwaambia wenzangu tubadilishe nguo kisha tukatoka na kutafuta bajaji.

“Nilimuomba dereva bajaji simu na kumpigia bosi wangu Junior Murder ili atupe ‘way forward’, akatuambia yeye na Ruge (Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji Clouds Media) tayari wamefungua kesi katika Kituo cha Polisi Oysterbay hivyo, tuelekee huko,” alisema.

Hata hivyo, alisema hawezi kuzungumza zaidi kwa sababu suala hilo bado liko kwenye upelelezi.

“Kuna watu wanadhani tunatafuta ‘kiki’, hii inatuumiza sana, tumelia, tuna hofu tunarudije kwa jamii…Bin Laden hayuko sawa na anashtuka mpaka anawashtua watu wote,” alisema.

MAZINGIRA YA STUDIO

Msanii huyo, alisema  mazingira ya studio hiyo tangu mwaka 2007 alipoanza kwenda ni salama na hakukuwahi kutokea uvamizi ama tukio lolote la hatari.

 “Pale ilipo studio ni kama nyumbani nimekuwepo kwa zaidi ya miaka 10, ni nyumbani kwa Jaji Lewis Makame (marehemu), eneo lile ni salama sana, kuna majirani ambao wanatupa amani, kuna Tibaigana (Kamanda mstaafu wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam), Waitara na mstaafu mmoja wa Magereza, Nanyaro.

“Kwa miaka yote tumekuwa salama, pamoja na hayo yote bado yametukuta hayo yaliyotokea. Kama sisi tumeweza kufanyiwa haya katika nyumba ya mtu mwenye heshima je, yule anayefanya shughuli zake kwingineko itakuwaje? alihoji Roma.

MWAKYEMBE

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, aliagiza uchunguzi wa suala hilo ufanyike haraka apatiwe majibu kabla hajawasilisha bajeti ya wizara yake.

“Nalifuatilia suala hili kwa karibu zaidi, nataka nipate majibu kabla sijawawasilisha bajeti yangu kwa sababu nataka ipite bila makelele.

“Nimeacha kazi zote na kuja hapa kwa sababu hata mimi nilikuwa nasumbuliwa, tumeshtushwa hali hii si ya kawaida kwa Watanzania, lazima tutafute kiini chake ni nini…watu wanataka kutuvuruga.

“Wasanii ndio wanaibrand (kuitangaza) Tanzania, siwezi kukubali wakachezewa chezewa tu, vyombo vya dola vifanye upelelezi tupate majibu ya kina,” alisema Dk. Mwakyembe.

MASWALI TATA

Kuna wakati waziri huyo alijikuta akishindwa kumudu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari, hatua iliyosababisha waandishi kumlalamikia.

Baadhi ya maswali hayo, ni nile linalomuhusu Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe, ambaye jana asubuhi alilitaka Bunge liahirishe shuguli zake na kujadili tatizo la utekaji watu alilosema linaharibu sifa ya nchi.

“Umeleta masuala ya kina Bashe, mimi hapa Mwakyembe, mambo hayo yako bungeni, hatuko hapa kujibu ramli,” alisema Dk. Mwakyembe.

Baada ya majibu hayo, waandishi wa habari walisikika wakisema ‘jibu swali, tumesubiri tangu saa 8 mchana mmekuja kuzungumza saa 9:30 alasiri, halafu mnasema mna haraka mbona sisi tumewasubiri’.

Swali lingine ni lile linalomuhusu kiongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye alisema Roma ataonekana kabla ya Jumapili na kweli akaonekana.

“Siwezi kujibu kwa ‘ear say’ na mkiendelea kupiga kelele kama watoto wa shule naondoka hapa…siwezi kuamini mpaka nione ‘recording’ ya huyo kiongozi,” alisema.

Hata baada ya kupewa sauti ya kiongozi huyo Dk. Mwakyembe hakuweza kutoa majibu ya kutosheleza.

Roma, aliwasili Maelezo saa 9:30 alasiri akiwa kwenye gari lenye namba za usalji T 589 BSA, aina ya Toyota Land Cruiser V 8.

Baada ya mkutano kumalizika saa 10:18 jioni, aliongozana na Dk. Mwakyembe hadi ofisini kwake ambako walikaa hadi saa 11:00 jioni alipotoka na kuondoka.

[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=TWgrN-XPMD0[/embedyt]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles