26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

WABUNGE WAHOFIA MAISHA YAO

*Bashe atonywa na mawaziri atapotea na wenzake 11


Na Fredy Azzah-DODOMA

HOFU imetawala kwa wabunge kutokana na kuibuka kwa matukio ya utekaji huku Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), akisema ameambiwa na baadhi ya mawaziri kuwa yeye ni kati ya wabunge 11 ambao wakikaa vibaya  wanaweza kupoteza maisha.

Hoja hiyo aliibua jana bungeni mjini hapa, baada ya kipindi cha maswali na majibu ambapo mbunge huyo aliomba mwongozo wa Spika kwa kutaka Bunge liahirishe shughuli zake zote ili wabunge waweza kujadili matukio hayo ambayo yanawafanya wananchi kila kona kuwa na hofu.

Hoja hiyo ya Bashe iliungwa mkono  na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) ambaye naye aliomba mwongozo kupitia kanuni ya 47 na kusema hali ya usalama kwa wananchi sasa hivi ni ya wasiwasi.

Hata hivyo hoja hizo zilikataliwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ambapo wabunge waliweza kuchangia kupitia michango yao wakati wa kuchangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu matukio hayo ya utekaji nchini.

katika mwongozo wake huo Bashe alisema. “Kumekuwa kukitokea matukio ya sintofahamu na si tu kuhusu wabunge, hata raia, kumekuwa na kikundi ambacho kimekuwa kikiteka watu.

“Miongoni mwa watu waliowahi kutekwa ni Mheshimiwa Msukuma (Joseph Msukuma, Mbunge wa Geita Vijijini) Mheshimiwa Bashe (Hussein Bashe), kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, ndugu Malima (Adam Malima, aliyekuwa Mbunge wa Mkuranga).

“Ben Saanane (Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema) amepotea, juzi ametekwa ndugu Roma Mkatoliki (Msanii Ibrahim Mussa) na Mheshimiwa Naibu Spika, nasema ni jambo la dharura kwa sababu hawa ni wale ambao wanafahamika, hatujui ni Watanzania wangapi hawafahamiki katika ngazi za chini.

“Zipo taarifa ambazo binafsi nimezipokea kutoka kwa baadhi ya mawaziri wakinitahadharisha mimi binafsi kwamba, Bashe kuwa makini wewe ni mmoja kati ya wabunge 11 ambao wamewekwa katika list (orodha), mkikaa barabarani vibaya, mnaweza kupoteza maisha yenu.

“Mheshimiwa Naibu Spika jambo hili ni dharura kwa sababu, kikundi hiki kilichomo ndani ya (anataja moja ya taasisi ya mambo ya usalama), ambacho kimeamua kuchukua mamlaka haya ya kuteka watu, kinaharibu heshima ya Serikali yetu, kinaharibu heshima ya chama changu, ambacho mimi na wabunge wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tuliomba ridhaa ya kutaka kuwaongoza Watanzania na si kuwahatarishia maisha yao.

“Kwa hiyo naomba mheshimiwa Naibu Spika, uruhusu jambo  hili tulijadili kama Bunge na ikikupendeza Bunge hili liunde Committee (kamati) maalumu ya kuweza kuchunguza jambo hili linaloendelea katika nchi yetu.

“Ama kuiagiza Kamati ya Usalama na Mambo ya Nje ya Bunge hili,  iweze kufanya kazi yake na kutuletea taarifa kwa ajili ua usalama wa wananchi wa nchi hii, hali ya nchi siyo salama, Watanzania wana taharuki, Watanzania wanajadili mambo haya katika mitandao, na there is no statement ya hope (hakuna kauli ya matumaini) kutoka serikalini,” alisema Bashe.

Pamoja na hpja hiyo kabla hajamaliza maelezo yake, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia, alimkatisha na kumtaka akae chini..

“Mheshimiwa Bashe naomba ukae, kaununi ya 47 inanitaka nikupe nafasi ya kutoa hiyo hoja,” alisema Dk. Tulia

Sugu

Kwa upande wake Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph  Mbilinyi ‘Sugu’, alisema Taifa limekuwa gizani kwa utamaduni mpya uliozuka wa kuteka watu, utamaduni ambao si wa nchi bali ni wa kimafia.

Alisema utamaduni huo kwa mara ya mwisho ulikuwapo katika mipaka ya Bara na Zanzibar kwa kupotezwa Mzee Kassim Hanga.

“Lakini tangu kipindi hicho haujakuwapo tena. Toka operesheni hii ya kuteka watu nyara ianze, kila anayehusika na usalama likiwamo Jeshi la Polisi, always (kila wakati) wanasema 'hatujui, hatujawaona kwenye vituo vyote'.

“Nchi inabaki kwenye tahayari, kapotea Ben Saanane, mara miili sita, saba imeopolewa kwenye Mto Ruvu ikaenda kuzikwa bila kufanyiwa Post mortem (kufanyiwa uchunguzi) kwa amri ya ambaye hatujui ni nani.

“Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu Nchemba) yuko kimya mpaka najiuliza kama anabanwa kiasi hicho, huyu ni mtu potential (muhimu) ambaye alifikia hatua ya kugombea urais na bado ana future.

“Kwanini asijiuzulu akalinda heshima yake kuliko kukaa kwenye mess (aibu)?  kujiuzulu ni utamaduni mzuri. Mzee Mwinyi (Ali Hassan Mwinyi) alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani miaka hiyo, mwaka '76, ikatokea mess, aka-bounce back, miaka ya '80 akaja kuwa Rais wa nchi hii.

“Ndugu yangu Mwigulu nikushauri, kama hushirikishwi, mambo yanafanyika, hamna mtu anakuja na majibu. Lakini juzi baada ya kutekwa Roma Mkatoliki, tumepata mwanga. Yupo mtu Dar es Salaam alituambia anajua Roma aliko na angerudi kabla ya Jumapili.

“Kama Waziri Kivuli nikatoka Jumamosi na ku-demand kwamba aachiwe siku ileile na akaachiwa, nashukuru Mungu. Sasa basi, hatujui nani next (anayefuata) atatekwa. Yawezekana Sugu ingawa mimi I don't care much (sijali) kwa sababu Mbeya gape my gape.

“Lakini Naibu Spika it could be you (inaweza kuwa wewe). It is the war (ni vita), no body is safe (hakuna aliye salama).

“Kwanini Bunge hili lisijadili na hatimaye limlazimishe Bashite kama alivyojua kwamba Roma Mkatoliki yuko wapi na angemrudisha Jumapili, tumlazimishe sasa Bunge hili tujadili na baadaye tumlazimishe Bashite atutajie aliko Ben Saanane kwa sababu huyu anaonekana anajua undani wa mambo haya,” alisema Mbilinyi.

Dk. Tulia

Akijibu miongozo hiyo, Dk. Tulia alisema. “Waheshimiwa Bashe na Sugu wameeleza kwa kirefu kuhusu jambo ambalo limetokea hapa na pale lakini pia tumeliona kwenye vyombo vya habari na tumelisoma.

“Maelezo yao kwa ujumla yanahusu mambo ambayo yanawapata wananchi ambayo watu kadhaa wametajwa kama mifano kwamba wamekuwa wakitekwa ama wamekuwa wakikamatwa.

“Sasa, nadhani wote tunafahamu matakwa ya Kanuni ya 47, hili jambo la hawa watu kukamatwa ama kutekwa kwa sababu sasa hata wale waliokamatwa, na wao wamewekwa kwenye kundi la kutekwa. Sasa sijui kama tunaweza kuyatenganisha haya mambo mawili nani amekamatwa.

“Mheshimiwa Bashe amekwenda mbali zaidi akisema kwamba kipo kikundi ndani ya (anakitaja) ambacho kinafanya kazi hiyo.

“Na Mheshimiwa Joseph Mbilinyi na yeye ameeleza kwamba hili jambo sasa limekuwa kama utamaduni kwa maana ya kwamba linatokea kila wakati na akaenda mbele zaidi na kumshauri Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwamba aweze kujiuzulu akiona inafaa,” alisema.

Kutokana na hali hiyo alisema kanuni ya 47 ni lazima isomwe ya 48 ndiyo inayoweka masharti ya matumizi ya kanuni ya 47.

“Sasa kwa kuwa kanuni ya 48(4) nitaisoma, inasema hivi jambo lolote litahesabiwa kuwa ni lenye maslahi kwa umma iwapo utatuzi wake unategemea kuwa zaidi kuliko zile za utekelezaji wa kawaida wa sheria peke yake.

“Masuala haya yaliyoulizwa na mheshimiwa Bashe na pia yaliyoulizwa na mheshimiwa Mbilinyi yako chini ya utaratibu wa kisheria na Bunge hili litashughulika na mambo ambayo ni yenye masilahi ambayo sheria haina uwezo wa kuyatolea majibu.

“Kwa sababu hiyo, sitalihesabu hili jambo kwa mujibu wa Kanuni ya 47(4) kwamba ni jambo la dharura lakini ni jambo ambalo utaratibu wa kawaida wa kisheria unaweza ukafanya kazi,” alisema Dk Tulia.

Devotha Minja

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Minja (Chadema), alisema askari wenye silaha wamefika nyumbani kwake wakitaka kumkamata, ili hali hajui kosa lake.

Hayo aliyasema jana bungeni katika mwongozo wake aliomba kwa kutaka kujua kwanini agizo alilotoa Spika Job Ndugai, kwamba mbunge asikamatwe bila kiongozi huyo wa mhimili huo kutaarifiwa.

“Hivi karibuni mheshimiwa Spika alitoa mwongozo kuhusu kamatakamata ya wabunge. Jana (juzi) saa tano asubuhi, huko mkoani Morogoro nyumbani kwangu, watu ambao wanaojiita kuwa ni askari, wakiwa na gari la polisi, wakiwamo askari ndani ya gari hilo, wakiwa na silaha za moto, waliizunguka nyumba yangu kwa lengo la kunikamata,  familia yangu ilipohoji nina kosa gani, hawakujibiwa ila (askari) waliambiwa kwamba niko Dodoma kwa ajili ya shughuli za kibunge.

“Lakini Naibu Spika, nilijaribu kumpigia simu RCO (Mkuu wa Upelelezi) wa Mkoa wa Morogoro kumuuliza na akakiri kwamba alituma vijana kwenda kunikamata.

“Hivi sasa kuna kamatakamata za kila namna na watu wanapotea katika mazingira ya kutatanisha. Lakini vilevile, kitendo cha askari kwenda na silaha za moto na kuizunguka nyumba yangu kilisababisha sintofahamu hata kwa watoto wangu,” alisema.

Akijibu mwongozo huo, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema mwongozo huo umeombwa kwa kanuni ambayo haihusiki nao.

“Kwa hivyo si jambo ambalo mimi niliyekaa hapa, ninaweza kulitolea mwongozo kwa mujibu wa hii kanuni ya 68 (7). Kanuni ya 68 (7) inataka mwongozo uombwe kwa jambo lililotokea mapema bungeni.

“Kwa sababu hiyo, pamoja na maelezo kwamba mheshimiwa Spika aliwahi kutoa maelekezo kuhusu yeye kutaarifiwa, hapa hapa bungeni waheshimiwa wabunge, tuliisoma ile sheria inayohusu haki, kinga na madaraka ya Bunge na inaeleza kosa gani mbunge anapotakiwa kukamatwa, Spika atataarifiwa na ni makosa yapi ambayo mbunge anaweza kukamatwa bila Spika kutaarifiwa.

“Tulishasoma hapa na si lengo langu kurudia hivyo vifungu. Kwa hiyo, mwongozo wangu katika hili ni kwamba kanuni ya 68(7) inanitaka kutoa mwongozo kwa jambo lililotokea mapema bungeni na hili halijatokea bungeni,” alisema Dk. Tulia.

Mwigulu anena

Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, akizungumza na waandishi wa habari alisema inabidi watu watofautishe kati ya kutekwa na kukamatwa ingawa hata wanaokamata watu, inapaswa kuwaeleza wanawakamata kwa kosa gani.

 “Serikali ina mkakati wa kuhakikisha wananchi wanakuwa katika usalama wao wenyewe na mali zao na wananchi tunawaomba sana kuendelea kutoa ushirikiano ili kuwabaini watu wanaotenda mauvu,” alisema.

Kuhusu masuala ya utekwaji kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Roma aliyeonekana na Saanane ambaye ukimya umetawala alisema hayo ni masuala  ambayo yako katika ngazi ya kiuchunguzi, hawezi kuyazungumzia.

[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=TWgrN-XPMD0[/embedyt]

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles