26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Aliyemweka Mtanzania rehani Pakistan akamatwa

pakistani*Ni mfanyabiashara ‘Juma Neti’ wa Kunduchi

*Afikishwa mahakamani kwa kosa la kusafirisha binadamu

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

MFANYABIASHARA Juma Mwinyi maarufu (Neti) aliyekuwa akidaiwa kumweka reheni mdogo wake nchini Pakistani kwa Sh bilioni 1.5 afikishwa mahakamani kwa tuhuma za kusafirisha binadamu.

Juma alipanda kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka yanayomkabili mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha.

Akisoma mashtaka Wakili wa Serikali Mkuu, Peter Njike alidai kati ya Desemba Mosi mwaka 2015 na Julai 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam mshtakiwa alitenda kosa la kusafirisha binadamu kinyume cha sheria.

Njike alidai Juma  alijifanya anakwenda kumpa mafunzo Adam Akida Mkazi wa Magomeni, Mtaa wa Chemchem na Idirsa na badala yake alimsafirisha kwenda nchini Pakistan kwa ajili ya kumweka reheni.

Mshtakiwa alipotakiwa kujibu kama kweli ama si kweli, alikana kuhusika na tuhuma hizo na upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika wakaomba kuahirisha kesi.

Hakimu Mkeha alimfahamisha mshtakiwa kwamba shauri lake halina dhamana kisheria, anaamini upande wa mashtaka hautachukua muda mrefu kukamilisha upelelezi.

Baada ya kusema hayo, alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 17 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa alirudishwa rumande.

Hatua ya kukamatwa kwa Juma, ni matokeo ya gazeti hili kuripoti habari za Mtanzania kushikiliwa ughaibuni kutokana na biashara ya dawa za kulevya Julai 18, mwaka huu.

Habari hizo ziliripotiwa baada ya video kusambaa katika mitandao ya kijamii Julai 17, mwaka huu ikimwonesha Adamu Akida alivyowekwa chini ya ulinzi na maharamia hao wenye silaha.

MTANZANIA lilifuatilia tukio hilo na kubaini kuwa, Adamu alikuwa amewekwa rehani kwa gharama ya Sh bilioni 1.5 kwa kile kilichoelezwa kuwa ilikuwa ni utekelezaji wa mpango wa biashara ya ‘unga’.

Kutokana na hatua hiyo, timu ya MTANZANIA iliamua kuchimbua suala hilo ili kujua ukweli wa namna kijana Adamu Akida, alivyokuwa kwenye mateso hayo.

Akisimulia tukio hilo kaka yake aliyejitambulisha kwa jina la Hemed Abdallah (si jina lake halisi) alisema miezi minane iliyopita, Adamu alikwenda kwa kaka yake ambaye ni mtoto wa mama yake mdogo aliyetambulika kwa jina la Juma na kuomba msaada wa mtaji kwani kazi yake ya kinyozi haikuwa ikilipa na hali ya maisha ilikuwa ngumu.

Alisema baada ya kueleza shida yake, Juma alimuhoji kama yupo tayari kwa ajili ya kutafuta maisha nje ya nchi na Adamu alikubali kufanya kazi ya aina yoyote ili mradi aweze kupata fedha.

“Awali alikwenda kwa kaka yake mtoto wa mama yake mdogo anaitwa Juma na kuomba asaidiwe mtaji kwani amekuwa na maisha magumu sana. Baada ya hali hiyo aliambiwa kuna safari ya kwenda Pakistan ambayo waliondoka wakiwa wameandamana watu watatu pamoja na Juma na kijana mwengine ambaye jina lake limenitoka, ila anaishi Kinondoni.

“Walipofika kule, Juma akachukua mzigo akiwa na yule kijana wa Kinondoni, huku Adamu akiachwa Pakistan kwa maelezo kuwa baada ya siku tano atakuja nchini na mzigo mwingine. Muda wote hata tukihoji alipo Adamu tunaambiwa yupo anaendelea na kazi huko aliko na angerudi mwezi wa tisa au wa nane.

“Sasa hii video ndiyo imetupa picha halisi ya Adamu, maskini sijui kama tutampata akiwa hai. Hata hivyo kwa kipindi cha hivi karibuni, tulikuwa tukishangazwa na mwenendo wa Juma kwani amekuwa na fedha nyingi sana hadi kufikia kuwajengea nyumba dada zake pamoja na kuwanunulia magari,” alisema Abdallah huku akibubujikwa na machozi.

Kutokana na hali hiyo vyombo vya dola vilianza kuendesha msako wa ndani na nje ya nchi kumsaka Juma Neti, ambapo kutokana na hali hiyo ilielezwa kuwa walifika mara kadhaa nyumbani kwake Kunduchi Unonio kwa ajili ya kumsaka bila mafanikio, kwani alitoroka.

Mke alivyohama

Julai 19, mwaka huu chanzo cha uhakika  kililiambia MTANZANIA kuwa mke wa Adamu ambaye alikuwa akiishi Mtaa wa Sunna, Magomeni, alihamia Kijitonyama.

Mke huyo wa Adamu, alihamishwa na shemeji yake, Juma ambaye ndiye aliyempangia nyumba nyingine Kijitonyama.

“Katika suala hilo, tuna shaka kuwa hata mke wa Adamu anajua kinachoendelea, maana miezi mitatu iliyopita alihama Magomeni na kuhamia Kijitonyama, tena huku akisema mume wake karibu anarejea nchini.

“Lakini baada ya video kuanza kuonekana, sasa hata kupatikana hapatikani na hatujui amehamia nyumba gani huko Kijitonyama,” alisema Abdallah.

Kauli ya Mwenyekiti wa Mtaa

Akizungumza na Mtanzania, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Idrissa, Issa Mpangile, alisema askari kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi walifika katika ofisi yake na kumtaka waongozane kwenda katika nyumba ya baba mdogo wa Adamu.

Alisema walipofika nyumbani kwa Kessy Baharia Mtaa wa Idisa, ambaye ndiye baba mdogo wa Adamu, polisi walichukua maelezo yake na baadaye wakarudi katika ofisi ya Serikali ya Mtaa kuchukua maelezo yake.

Akizungumzia kuhusu kijana huyo, Mpangile alisema kuwa ni mzaliwa wa mtaa huo, lakini baadaye alihamia Mtaa wa Suna ambao ni jirani na Mtaa wa Idrissa, Kata ya Magomeni.

Alisema wakati kijana huyo anahama mtaa huo, alikuwa bado ni kinyozi na hakuwa na rekodi ya kusafiri kwenda nje ya nchi.

Alisema katika mazungumzo na Baharia, alimweleza kuwa amewasiliana na baba wa kijana huyo ambaye anaishi Bagamoyo mkoani Pwani.

Mpangile alisema kwa mujibu wa Baharia, baba wa kijana huyo anayejulikana kwa jina la Akida, amesikia habari za mtoto wake na kwamba atakwenda kuripoti kituo cha polisi.

Naye mama mdogo wa Adamu, aliyetambulika kwa jina la Khadija Katundu, alikiri maofisa wa polisi kumuhoji mume wake.

Alisema wameendelea kutoa ushirikiano kwa watu wanaofika nyumbani kwao kuhoji kuhusu suala hilo, na kwamba wanaamini ufumbuzi utapatikana.

Inasemekana kijana huyo aliwekwa rehani kwa ghamara ya Dola za Marekani 700, 000, sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.5 za Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa ndugu wa karibu wa Mtanzania huyo zinasema kuwa, Adamu aliwekwa rehani na kaka yake aitwaye Juma akitakiwa kulipa fedha za unga (mihadarati) aliyochukua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles