26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

TTCL yasambaza Mkongo wa Taifa mikoa yote nchini

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema hadi sasa limesambaza Mkongo wa Taifa katika mikoa yote nchini, ambapo zaidi ya wilaya 98 zimeunganishwa na mkongo huo wa mawasiliano. Juhudi hizi zinalenga kuhakikisha huduma za elimu, afya, na maendeleo ya kiuchumi zinapatikana kidigitali katika maeneo yote nchini.

Akizungumza leo, Julai 12, 2024, na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Tanzu ya TTCL (T-Pesa), Lulu Mkudde, alisema shirika linaendelea na mchakato wa kufikisha huduma zake za Mkongo wa Taifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikiwa ni muendelezo wa kupeleka huduma hiyo kwa nchi za jirani.

“Hadi sasa, huduma hii ya Mkongo wa Taifa imewafikishwa katika nchi nne, ikiwemo Burundi, Rwanda, Zambia, na Malawi,” alisema Mkudde.

Alisema kuwa lengo la kufungua milango ya kidigitali ni kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kutumia huduma za “Interneti” katika kutekeleza huduma mbalimbali.

“Hadi sasa, shirika limefanya mambo mbalimbali, ikiwemo huduma ya TTCL-Pesa ambapo katika Sabasaba hii tumekuja na huduma ya Akaunti Pepe, inayomuwezesha mteja kufungua akaunti yake bila hitaji la kuwa na benki, na kutumia akaunti hiyo masaa 24 kwa siku,” alieleza Mkudde.

Ameongeza kuwa TTCL inahakikisha huduma za mawasiliano zinakuwa bora ili kuwapa wananchi fursa ya kupata huduma mbalimbali za kujipatia kipato kupitia fursa hiyo ya Interneti kwa gharama nafuu.

Akizungumzia kuhusu huduma ya (T-Cafe), Mkudde alisema ni huduma ya WiFi inayowaondolea adha wafanyabiashara, waandishi wa habari, na wataalamu wa ushauri katika kufanya kazi zao wakiwa nje ya ofisi.

“Huduma hii inasaidia mtu yeyote kufanya kazi nje ya ofisi kwa kutumia Interneti kwa haraka na gharama nafuu. Katika kipindi hiki cha Sabasaba, tumeona jinsi huduma hii inavyofanya kazi kwa kasi ya hali ya juu na wananchi wameitumia sana katika maonesho hayo,” alisema.

Aidha, kupitia maonesho haya, TTCL imepata fursa ya kutoa elimu na kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu huduma wanazozitoa ambazo zinawafikia moja kwa moja.

“Tunawahimiza wananchi kuchangamkia fursa hizi za kidigitali ili kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani,” alihitimisha Mkudde.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles