Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Aliyekuwa mshambuliaji wa klabu ya Simba, John Bocco, ametambulishwa rasmi kuwa mshambuliaji mpya wa klabu ya JKT Tanzania. Bocco, ambaye ni kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Tanzania, tayari ameanza mazoezi na klabu yake mpya, akijiandaa kwa msimu ujao.
Msimu uliopita haukuwa mzuri kwa Bocco kutokana na kutopata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha Simba. Hata alipokuwa sehemu ya wachezaji wa akiba, nafasi yake ilichukuliwa zaidi na Jean Baleke na Moses Phiri. Katika msimu wa 2023/24, Bocco alicheza mechi tano pekee, akitumia dakika 185 uwanjani na kufunga mabao mawili tu.
Taarifa za kusajiliwa kwa Bocco zimewashtua wengi, kwani Juni 10, 2024, klabu ya Simba ilimtambulisha Bocco kuwa kocha wa timu yao ya vijana chini ya umri wa miaka 17, ambapo tayari alikuwa ameanza kazi hiyo. Bado haijafahamika kama ni ofa ya kuvutia kutoka JKT Tanzania ndiyo iliyomfanya Bocco kuacha kazi ya ukocha na kurudi kucheza soka au la.
Bocco anatarajiwa kuleta uzoefu wake na umahiri katika kikosi cha JKT Tanzania na kuwasaidia kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kwa msimu ujao.