28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Masauni aikosoa NIDA kwa kutotoa vitambulisho kwa wakati

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamadi Masauni, ameonyesha kuchukizwa na utendaji kazi wa Wakala wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kushindwa kutoa vitambulisho kwa wakati kwa wananchi, licha ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutoa shilingi bilioni 42.5 kwa ajili ya vitambulisho hivyo.

Waziri Masauni alitoa kauli hiyo Julai 10, 2024, wakati alipotembelea banda la NIDA katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa jijini Dar es Salaam. Alisema kuwa amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu upatikanaji wa vitambulisho, ikiwemo ukosefu wa mtandao na huduma kupatikana kwa watu wachache.

“Nakiri kuwa kwenye banda ambalo sijaridhika ni NIDA. Nimetembelea Uhamiaji, Magereza, Zimamoto na Polisi kote nimeridhika ila sijaridhika na NIDA kutokana na malalamiko mengi ya wananchi hata nje ya maonesho haya,” alisema Waziri Masauni.

Aliongeza kuwa alipokuwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, alikuta msongamano wa wananchi wakisubiri Kadi za NIDA. Alisema pia alishuhudia hali kama hiyo Mkuranga na Mburahati ambapo wananchi walilalamika sana kuhusu huduma za NIDA.

“Tatizo la ukosefu wa vitambulisho linatakiwa liwe historia kwa sababu kwa kipindi cha miaka miwili mitatu nyuma, nilikuwa naulizwa masuala mengi na wabunge,” alisema Masauni.

Waziri Masauni alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita ni sikivu na Rais Dk. Samia ametoa Sh bilioni 42.5 kwa ajili ya kununua vitambulisho ambavyo tayari vimechapishwa. Alikemea uzembe wa baadhi ya watendaji wa NIDA ambao wamekuwa wakiwazungusha wananchi katika kupata vitambulisho vyao.

“Ni kuitukanisha Serikali ya Mama Samia kumwambia mtu njoo kesho njoo kesho kufata kitambulisho chake kwa sababu ya uzembe wa watu wachache. Serikali imetoa fedha, vitambulisho vipo, na nilizindua mpango kabambe wa ugawaji wa vitambulisho ngazi ya Kata Mara,” aliongeza Masauni.

Waziri Masauni pia alitembelea banda la Polisi ambapo aliridhishwa na huduma zinazotolewa na taasisi za Magereza na Uhamiaji, ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu jeshi hilo. Alisema kuwepo kwenye maonesho hayo kuna wapa fursa wananchi kulijua jeshi la polisi na kupata elimu ambayo walikua hawaijua hapo awali.

“Kwenye banda la Polisi nimeshuhudia mabadiliko kwenye utendaji wa polisi na limeakisi dhamira njema na mwelekeo wa serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuona jeshi la polisi linakua la kisasa,” alisema Waziri Masauni.

Aliongeza kuwa matumizi ya mifumo yamekua na mafanikio hasa katika utoaji wa huduma pamoja na uwekezaji wa mifumo mingine kutoka nje ya nchi. Mfumo huo unaunganisha taasisi zingine pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali wa jeshi la polisi kushuhudia kesi zinapofunguliwa na hatua ambayo imefikiwa jambo ambalo linaimarisha uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles