Na mwandishi wetu.
Wananchi wa jamii ya kimasai wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro wamefanya tamasha la kimila la kiutamaduni huku wakisema kwamba wataendelea kuhama kwa hiyari kuelekea katika Kijiji cha Msomera na maeneo mengine nchini Tanzania.
Kufanyika kwa tamasha hilo la kiutamaduni ambalo limehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu wa kabila hilo limefuta taarifa za uzushi za baadhi ya taasisi zinazojiita kuwa zinatetea haki za binadamu ambazo zimekuwa zikidai serikali ya Tanzania imekuwa ikiwahamisha kwa kuwalazimisha na kutumia nguvu kuinyanyasa jamii hiyo,
Katika tamasha hilo la kiutamaduni jamii hiyo kuanzia katika rika la ujana wakiongozwa na wazee waliweza kufanya matambiko ya kimila ndani ya kreta bila kubughudhiwa na mtu yoyote na kuelezwa kwamba tukio hilo hufanyika kila baada ya miaka kumi.
Wakizungumza katika tukio hilo lililofanyika ndani ya kreta ya Ngorongoro badhi ya wananchi wa jamii hiyo wamesema wanaishukuru serikali kwa kuendelea kuwapa elimu ya kuhama kutoka ndani ya hifadhi kwenda Msomera na maeneo mengine na wataendelea kuhama kadri elimu inavyotolewa.
“Kwa ujumla tukio hili la leo linaiambia dunia kwamba serikali ya Tanzania haitumii nguvu katika kutuhamisha kutoka humu ndani ya hifadhi na ndiyo maana tuna furaha ingawa akili yetu yote ipo Msomera ili kuungana na wenzetu ambao tayari wameshahama.”alisema mwananchi mmoja ambaye alishiriki tamasha hilo na kukataa kusema jina lake.
Mmoja wa kiongozi wa kimila ambaye naye hakutaka kutajwa jina lake kuogopa kutengwa alisema tukio kama hilo pia linaweza kufanyika katika eneo lolote lile la nchi na sasa wanaendelea kuelimishwa na wenzao ili watoke kwenye eneo la hifadhi na kwenda Msomera na maeneo mengine yaliyotengwa na serikali.
Kufanyika kwa tukio hilo la kimila ambalo kwa mujibu wa jamii ya kimasai hufanyika takribani kila baada ya miaka kumi limewavunja nguvu baaadhi ya mashirika yanayodai kutetea haki za binadamu kwani madai yao ya jamii hiyo kuzuiwa kufanya shughuli yoyote ndani ya hifadhi yanaonekana kuwa ni ya uongo.
Mashirika hayo yamekuwa yakidai kwamba jamii ya wamasai nchini Tanzania imekuwa ikishurutishwa kuhama kutoka eneo hilo la tarafa ya Ngorongoro na kuhamia katika Kijiji cha Msomera na maeneo mengine yaliyotengwa na serikaii.
Hata hivyo serikali ya Tanzania imekuwa ikipuuza tuhuma hizo ambazo mara nyingi zimekuwa zikitolewa na mashirika wanaowatumia jamii ya kimasai kama chanzo cha kupata fedha badala ya kujali maendeleo yao ya kila siku.
Jamii ya kimasai ndani ya hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikiishi katika maisha magumu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanyama pori na hivyo kusababisha mauaji ya binadamu hasa Watoto wadogo na wanawake na hivyo kuhatarisha maisha yao,
Serikali iliamua kuwahamisha kwa hiyari wananchi kutoka ndani ya hifadhi ili kuwanusuru na vifo vya mara kwa mara vinavyotokana na ongezeko kubwa la wanyama wakali linalochangiwa pia na ongezeko la idadi ya watu ambapo uamuzi huo kwa sasa umepunguza vifo vingi.