Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mrembo anayefanya vizuri kwenye sekta ya mitindo nchini Kongo DRC, Benita Kanjinga Tshimi, amesema kiu yake ni kuleta uamsho katika tasnia hiyo Afrika Mashariki kwa kutumia wabunifu wachanga, mafundi cherehani na wadau wengine.
Benita ni Jaji mkuu katika maonyesho makubwa ya mavazi ya Afa Fashion Night yatakayofanyika Jumapili wiki hii katika ukumbi wa Golden Memory Classic Hall Dar es Salaam.
Akizungumza na mtanzania.co.tz Benita alisema anaamini kwa kutumia wabunifu wachanga ataleta uamsho mkubwa kama ambavyo nchi kama China ilivyo na mafanikio kwenye tasnia ya ubunifu.
“Ufundi cherehani (kushona) sio kwa wale waliofeli maisha, ufundi ni kazi inayotakiwa kutambulika sababu inasaidia na kuinua watu na sasa tupo kwenye kupromoti hiyo sekta itoke nje ya Tanzania, Kongo DRC, Kenya na kwingineko.
Nashukuru wabunifu wa Tanzania wameniunga mkono ili kuleta uamsho kwenye sekta mpaka tufike kwenye levo ya ‘made in Tanzania’ sawa na China wanavyofanya ‘made in China hivyo tutahitaji mafundi nguo wa mtaani wenye vibanda, wabunifu wote maana Mama Samia(Rais wa Jqmhuri ya muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan) ametusaidia kutangaza utalii hivyo natamani watalii wanavyokuja wanunue bidhaa zetu za mitindo kama nguo, viatu vyenye made in Tanzania,” amesema Benita.