24.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kampuni za China zakaribishwa kuwekeza sekta ya nishati

Na Mwandishi wetu

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian ambapo walizungumza masuala mbalimbali ikiwemo uhusiano uliopo kati ya nchi hizi mbili na uwekezaji kwenye  miradi ya nishati.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Novemba 24, 2023 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Ubalozi wa China nchini Tanzania wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Dk.Biteko, amemweleza Balozi Mingjian kuwa Tanzania inathamini uhusiano mzuri ulipo kati ya nchi hizi mbili ambao mwakani utafikia miaka 60 huku akitaja miradi mbalimbali kwenye sekta ya nishati na madini ambapo kuna wawekezaji na wakandarasi kutoka China.

“ Sisi Tanzania tunaufurahia na kuuthamini uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi yetu Tanzania na China, hapa kuna kampuni nyingi kutoka China zinazofanya kazi kwenye uchimbaji madini ikiwemo madini ya viwandani na uchenjuaji madini, pia kwenye miradi ya nishati kuna kampuni za Kichina zinafanya kazi mfano kampuni ya TBEA inayojenga laini ya umeme ya kV 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, na mradi wa kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Tanzania kwenda Zambia,” amesema Dk. Biteko.

Kuhusu miradi hiyo ya usafirishaji umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma na mradi wa TAZA, ametoa wito kwa serikali ya China kuiwezesha kwa namna mbalimbali kampuni hiyo ikiwemo kifedha ili itekeleze miradi hiyo kwa ufanisi na kwa wakati kutokana na umuhimu wake.

Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amesema kuwa, nchi ya Tanzania bado ina uhitaji wa umeme wa kutosha utakaotokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo maji hivyo amekaribisha kampuni kutoka China kuja kuwekeza kwenye eneo hilo.

Amemweleza pia Balozi, Mingjian kuhusu mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ambapo ameeleza kuwa nchi ya Uganda na Tanzania zinauthamini mradi huo na zinaendelea na utekelezaji wake ambapo kampuni kutoka China ya CNOOC ni moja ya wabia wa mradi huo.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini, Chen Mingjian naye ameeleza jinsi China inavyouthamini ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China na kueleza kuwa, kielelezo cha uwepo wa  ushirikiano huo mzuri ni ujio wa Rais wa nchi hiyo nchini Tanzania mwaka 2013 na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Rais wa Tanzania, Dk, Samia Suluhu Hassan na Rais wa China, Xi Jinping.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles