28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mkuu awapongeza watumishi wa Mahakama kwa utekelezaji wa mpango wa utoaji haki

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma amewapongeza Watumishi wote wa Mhimili huo kwa utekelezaji thabiti wa Mpango Mkakati na Programu za Maboresho zinazolenga kuboresha huduma za utoaji haki nchini.

Hayo amezungumza leo Mei 18, na Profesa Juma wakati akifungua Kikao cha siku mbili cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa PSSSF jijini Dodoma.

“Kabla sijafungua kikao hiki muhimu, nitakosa fadhila na uungwana kama nitashindwa kuchukua nafasi hii kuwapongeza wafanyakazi kwa ufanisi ambao umejipambanua katika kufanikisha na kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi,” amesema Jaji Mkuu.

Amesema ili kuendelea na maboresho ya huduma za Mahakama, Viongozi hawana budi kutambua nafasi na umuhimu wa Wafanyakazi, kwa kuwashirikisha kwa namna mbalimbali katika kupanga na kutekeleza kwa kadri ya uwezo wao.

“Hapa madhumuni makubwa ni kuleta ufanisi na tija zaidi kazini na pia kuondoa migongano isiyo ya lazima, kuwashirikisha wafanyakazi ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanaelimishwa mara kwa mara kuhusu masuala yote muhimu ya Mhimili wa Mahakama yanayojitokeza kila siku,” amesema Prof. Juma.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania amewataka Watumishi hao kusoma Rasimu ya Taarifa ya REPOA ya Utafiti Kuhusu Kuridhika Kwa Watumiaji wa Huduma za Mahakama (Court User Satisfaction Survey) 2023.

“Katika karne hii tuliyo nayo ni muhimu kuwa na desturi ya kujisomea ili kuendana na mabadiliko ya Teknolojia na vilevile nawaomba hao kuwa na desturi ya kupenda kujisomea nyaraka mbalimbali zitakazowezesha kujua zaidi kuhusu maboresho ya kufanya,” amesisitiza Prof. Juma.

Amesema, kwa mujibu wa Rasimu ya taarifa hiyo aliyoisoma, inaonesha kuwa, tathmini ina mwelekeo mzuri ambapo amesema: “Kumekuwa na ongezeko thabiti la kiwango cha kuridhika na wepesi wa kuwasikiliza, heshima na adabu inayoonyeshwa na wafanyakazi wa mahakama kutoka 2015 hadi 2023.”

Akizungumzia safari ya maboresho ya Mahakama, Jaji Mkuu amesema TEHAMA imechangia kwa kiasi kikubwa huku akiendelea kusisitiza kuhusu matumizi ya Teknolojia kwa vitendo ili kutimiza azma ya kuwa na Mahakama mtandao (e-Judiciary).

“Ndugu Wajumbe na wageni waalikwa, naomba nitumie Baraza hili kutambua mchango mkubwa katika kuleta ufanisi uliotokana na matumizi ya TEHAMA. Nitumie pia Baraza hili kuendelea kukumbushana kuwa utoaji wa huduma kwa umma katika Karne ya 21 ni tofauti kabisa na ilivyokuwa miaka michache,”amesema Profesa Juma.

Amesema watumishi wasiridhike na elimu na ujuzi walionao na badala yake kujiendeleza na kujisomea nje ya taaluma zao ili kuwa na uwezo wa kufanya kazi nyingi nje ya taaluma iliyowapa ajira (multi-task).

“Jitihada binafsi za watumishi ndio zitaiwezesha Mahakama kuhimili pengo kubwa la idadi ya watumishi. Mahakama inahitaji watumishi 10,351, waliopo ni 6,000, sawa na asilimia 58. Karne ya 21 ni ya ubunifu. Kila mtumishi kwa nafasi yake, anatakiwa kuwa mbunifu na kuongeza thamani katika kazi anazofanya,” amesisitiza.

Amesema, Kikao cha Baraza, ni wakati mzuri wa kubadilishana uzoefu katika kukabiliana na changamoto, kukumbushana hatua iliyofikiwa tumefika na kujua wapi panahitaji kujirekebisha pamoja na kuwaelimisha watumishi kuhusu masuala mbalimbali yanayogusa maslahi na haki zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles