Na Suleiman Rashid Omar-Pemba
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imesema haitowavumilia watu wanaowatumia wanafunzi wa shule za sekondari kwa kuuza dawa za binadamu hali ya kuwa hawana taaluma hiyo.
Onyo hilo limetolewa na Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Afya Kisiwani Pemba, Bakari Ali Bakari, alipokuwa shehena za dawa mbalimbali zilizotolewa na UMATI kisiwani hapa ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa uimarishaji afya kupitia huduma Lishe, Uzazi na Usafi wa Mazingira.
“Ni jambo lisilokubalika kwa baadhi ya wamiliki wa maduka ya madawa kuwaweka watoto wao washule kuuzia watu madawa sisi kama wizara ya afya tutahakikisha wale wote wenye mtindo huo tunawakamata,” Bakari
Kutokana na hali hiyo aliiagiza Bodi ya Madawa kufanya ukaguzi kila wakati ili kuhakikisha kila kituo cha afya vikiwemo vinavyomilikiwa na watu binafsi vinafuata masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake Mratibu wa UMATI kisiwani Pemba, Rashid Abdalla Rashid, alisema lengo la kukabisdhi dawa hizo ni kusaidia vituo vya afya vilivyo ndani ya mradi huo.
Alisema mradi huo una lengo la kuboresha afya ya uzazi na kupunguza ongezeko la maradhi ya kuambukiza pamoja na Vifo vya watoto katika mkoa wa kaskazini Pemba
Akivitaja vituo vitakavyopatiwa madawa hayo kuwa ni Maziwang’ombe, Shumba, Vyamboni, Konde na Hospitali za Micheweni, Kojani, Tungamaa, Jadida na Hospitali Wete.
Alisema wakati wa kutekeleza mradi huo inatarajia kujenga vyoo katika Shule ya Kojani na kuweka tangi la maji ilikuondoa tatizo la maji katika shule hio.