WASHINGTON, MAREKANI
MAAMBUKIZI ya virusi vya corona dunianiani yamefikia zaidi ya watu milioni mbili jana, kwa mujibu wa taarifa ya Chuo Kikuu cha Afya cha John Hopkins cha nchini Marekani.
Katika hao, taarifa hiyo inaeleza kuwa zaidi ya watu 119,500 tayari wameshariporiwa kufariki dunia na wengine zaidi ya 450,000 wameshapona baada ya kupata maambukizi.
Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) linatarajiwa kutoa ushauri rasmi wa kimkakati kuhusu namna ya kukabiliana na virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 utakaojumuisha njia sita muhimu za kuzuia watu kutembea na kuchangamana.
Hadi sasa, takwimu zinaonesha kuwa Marekani ndiyo inayoongoza kwa idadi kubwa ya maambukizi yanayofikia zaidi ya watu 581,000 na tayari watu 23,000 nchini humo wameshafariki dunia.
Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka na Jiji la New York ndilo lililoathirika aidi likiwa na vifo vya zaidi ya watu 10,000.
Tayari majimbo kadhaa nchini humo yamelazimika kutangaza amri ya dharura, kufunga shule na biashara zote, huku watu wakihamasishwa kutochangamana na kujiweka karantini kwa muda.
Pamoja na hatua zinazochyukuliwa, kwa jana angalau kulikuwa na ahueni baada ya taarifa kuelea kwamba vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Covid-19 havijaongezeka Marekani
Kwa mara ya kwanza ilielezwa kwamba idadi ya vifo kutokana na virusi vya corona nchini humo haikuongezeka kwa siku ya pili mfululizo, ambapo gavana wa mji wa New York alisema hali mbaya sasa imekwisha, wakati nchi nyingi zikitafakari kufungua taratibu uchumi wao uliovurugika.
Tangu kuzuka kwa virusi hivyo mwaka jana, janga hilo la corona limesababisha maambukizi, vifo na kuielekeza dunia katika mdororo mkali wa kiuchumi wakati zaidi ya nusu ya wakazi duniani wakibakia majumbani mwao.
Hata hivyo, Rais Donald Trump wa Marekani amedai kuwa na mamlaka kamili ya kuamua vipi na lini uchumi wa nchi hiyo unaweza kufunguliwa baada ya wiki kadhaa za miongozo ya hatua kali za watu kujitenga kwa lengo la kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.
Lakini magavana wa majimbo kutoka vyama vyote wamejibu haraka, wakieleza kwamba wana wajibu wa msingi wa kuhakikisha usalama wa umma katika majimbo yao na wataamua lini hali ni salama kuanza kurejea katika hali ya kawaida.
Trump hakutoa maelezo juu ya chanzo cha madaraka yake hayo, ambayo anadai, licha ya ukomo wa kikatiba, uliopo.
Matamshi hayo yalikuja muda mfupi baada ya viongozi wa chama cha Democratic katika pwani ya kaskazini mashariki na magharibi kutangaza juhudi zao za ushirikiano kupunguza amri ya kubakia nyumbani ama kufungua biashara kwa mujibu wa muda wanaoona unafaa.
Wakati nchi zikifikia viwango tofauti vya maambukizi ya virusi vya corona, mjadala unaendelea kuhusu kurejea katika hali ya kawaida na uwezekano wa kuzuka tena wimbi kubwa zaidi la maambukizi.
Lakini Italia na Austria zinafungua upya baadhi ya maduka na Hispania inaanza ujenzi na kazi za viwandani wakati Ujerumani inapima uwezekano wa kuruhusu uchumi wa nchi hiyo kuanza tena.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema jana kuwa hatua za kuwazuia watu kubakia majumbani mwao zilizoanza kutumika Machi 17 zitaendelea hadi Mei 11.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi alisema pia jana kuwa hatua za kuzuwia watu kutoka nje nchini humo, ambazo zimewalazimu watu wapatao bilioni 1.3 kubaki majumbani mwao, zitarefushwa hadi Mei 3.
Hatua hiyo inakuja licha ya malalamiko kutoka kwa mamilioni ya watu masikini ambao wamebaki karibu bila msaada wowote wakati ajira zimetoweka na mapato yamekauka.
Modi alisema kuwa kwa mtazamo wa kiuchumi, India imepata pigo kubwa, lakini maisha ya watu wa India yana thamani kubwa zaidi.
Modi alisisitiza kuwa inawezekana kulegeza vizuwizi kuanzia Aprili 20. Hatua za hivi sasa za wiki tatu za kuzuia watu kutoka nje nchini India zilizowekwa tangu Machi 25 zilitarajiwa kumalizika usiku wa manane jana. India ina kesi 10,000 za maambukizi na vifo 339.