Ramadhan Hassan
BUNGE limeelezwa kuwa Wizara ya Kilimo ipo katika hatua za mwisho kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Maendeleo ya Ushirika yatakayoendana na mahitaji ya sasa.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbinga Mjini, Martini Msuha (CCM) ambaye alitaka kujua kuwa Serikali ina mpango gani wa kurekebisha Sheria ya Vyama vya Ushirika ili kuondoa mapungufu yaliyopo.
Akijibu swali hilo, Bashe alisema mabadiliko hayo yatahusisha mfumo na muundo wa uongozi ili kuendana na mahitaji ya teknolojia na kuleta ushindani wa kibiashara.
“Tunaelewa kuwa ushirika ni dhana ya hiari, lakini Serikali ni msimamizi mkuu wa vyama vya ushirika pale ambapo viongozi wake au vyama vyenyewe havitekelezi malengo yaliyokusudiwa na ushirika.
“Tunakiri vyama vinakabiliwa na changamoto za kiutendaji, usimamizi, viongozi kutokuwa waadilifu na mapungufu ya kimfumo ya uendeshaji wa vyama vya ushirika hapa nchini,” alisema Bashe.
Aidha, Bashe alisema vipo baadhi ya vyama vya ushirika ambavyo vinafanya vizuri.
“Mfano, Chama cha Ushirika cha Chai Mkonge, Mafinga na Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU), ushirika ndicho chombo cha kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi kwa kuwaunganisha wakulima ili kuwa na nguvu ya pamoja katika kutoa huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo na kutafuta masoko ya mazao,” alisema Bashe.
Hata hivyo, alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2015 – 2020 (Ibara ya 22 (g)(iv) na 86 (a), inaelekeza kuifanyia mapitio sera ya vyama vya ushirika na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Ushirika na upatikanaji wa takwimu zitakazosaidia kuandaa mipango.
“Nyingine ni kuleta mageuzi katika sekta ya ushirika na kuimarisha uchumi wa taifa na kuviimarisha vyama vya ushirika kuwa na uwezo wa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ya ndani na nje kwa kuweka mfumo madhubuti wa ukusanyaji, uchambuzi na uenezaji wa taarifa za masoko na kutoa elimu juu ya uongezaji thamani na biashara,” alisema Bashe.