25.5 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Kashaba wanufaika mradi wa maji

Nyemo Malecela – Kagera


WAKAZI wa Kijiji cha Kashaba, Kata Kyaka, Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, wamesema wamekuwa wakilala bila kuoga na wakati mwingine wakilazimika kutumia maji waliyofulia nguo kunawa miguu, kutokana na kijiji hicho kukumbwa na uhaba wa maji.
Wakizungumza wakati wa kukabidhiwa rasmi mradi wa maji uliojengwa na Shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Kagera kwa kushirikiana na jamii ya kijiji hicho, wenye thamani ya Sh milioni 192, wananchi hao walisema kuwa mradi huo ni faraja kwao kwani utaziokoa familia nyingi zenye kipato duni.
Vesta Emmanuel, mkazi wa kijiji hicho alisema wameteseka kwa muda mrefu kutembea kati ya kilomita tatu hadi tano kufuata maji na kuwa wakati mwingine walilazimika kutumia maji ya madimbwi.
“Mtu akichota madumu mawili, anatoa dumu moja kwa ajili ya kupikia, kama ana mtoto mchanga atatumia moja kufulia nguo za mtoto na maji aliyofulia anaamua kunawa miguu, maana hawezi kupata maji ya kuoga,” alisema Vesta.
Naye Agnes Leonard mkazi wa kijiji hicho, alisema kuwa matumizi ya maji ya madimbwi yaliwasababishia magonjwa kama kichocho, hali iliyosababisha kupoteza muda mwingi kwenda hospitali badala ya kufanya shughuli za uzalishaji mali.
“Kuna wakati watoto wetu walishindwa kwenda shule ili wasaidie wazazi wao kwenda kuchota maji kwa matumizi ya nyumbani, hali hii ilisababisha maendeleo yao kielimu kurudi nyuma, tunaishukuru World Vision kutuletea maji, sasa tutatumia majisafi na salama,” alisema Agnes.
Kwa upande wake, Mratibu wa mradi wa World Vision Missenyi AP, Renatus Rugakingira aliwataka wakazi hao, hasa wanawake kuutumia mradi huo kujiinua kiuchumi kwa kuanzisha kilimo cha mboga mboga.
Alisema kuwa mradi huo unaolenga kunufaisha wananchi 2,897 ulianzishwa mwaka 2018 na kukamilika Septemba mwaka jana na kuwa lengo lake ni kuwanusuru wanawake na watoto ambao walifuata maji mbali ambayo pia hayakuwa salama.
“Katika mradi huu, World Vision ilitoa shilingi milioni 190, lakini pia wananchi walichangia nguvu zao, ikiwamo kuchimba mitaro, kusomba mawe na kutoa eneo kwa ajili ya mradi,” alisema Rugakingira.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Innocent Mukandala ambaye ndiye alikabidhiwa rasmi mradi huo, aliwataka wananchi kulinda na kutunza miundombinu ya maji ili iwe endelevu na kuwa Serikali haitakuwa tayari kusikia imeharibiwa.
Aidha aliwataka wananchi kuchangia Sh 1,000 kwa kaya kila mwezi kwa uendeshaji na matengenezo ya vifaa vitakapoharibika.
“Huu mradi unatumia vifaa, msipochangia itafika wakati vitaharibika na hela ya kuvikarabati itakosekana, sasa kama hamjachanga itatoka wapi au mtarudi tena World Vision kuwa tutengenezewe vifaa vimeharibika?” alihoji Mukandala.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles