BEATRICE KAIZA
MREMBO anayefanya vyema kwenye tasnia ya filamu za Kibongo, Wema Sepetu, wiki hii amekuwa gumzo baada ya picha yake kusambaa mtandaoni ikimwonyesha amepungua mwili tofauti na ilivyozoeleka.
Swaggaz tumepata nafasi ya kufanya mahojiano ‘X-clusive’ na Wema Sepetu ambaye jana alitangazwa kuwa balozi wa bidhaa za nywele chapa, Angels Hair Collection na hapo chini anafunguka mengi kuhusiana na mwonekano wake mpya.
SWAGGAZ: Kuna warembo wengi hapa Bongo, unadhani kwanini dili hili la ubalozi limekuja kwako?
Wema: Nimepata hili dili kutokana na ubora wangu, nina mashabiki wengi pia mimi huwa nafanya kazi na kampuni zenye bidhaa bora, siwezi kufanya kazi na watu wenye bidhaa mbovu na nitakuwa balozi kwa muda wa mwaka mmoja lakini nitaendelea kufanya nao kazi sababu wana bidhaa nzuri.
SWAGGAZ: Wiki hii umekuwa gumzo mtandaoni baada ya mashabiki zako kukushambilia kwa kuwa umepungua sana, je ni kweli unaumwa?
Wema:Kitu cha kuwaambia mashabiki zangu ni kwamba mimi ni mzima wa afya, sina ugonjwa wowote na kuhusu mashabiki kunitukana kuwa nimepungua sana, nimeshawazoea kwani hapo nyuma nilinenepa na nilikuwa nasemwa pia.
SWAGGAZ: Lakini kwanini umekuwa ukiwajibu mashabiki zako kwamba umepungua sababu una Ukwimwi?
Wema:Ukiona nimemjibu shabiki kwenye picha ambayo nimeweka mtandaoni ni kwa sababu ya maneno yao, mimi pia nina moyo kuna maneno mengine yanauma.
Pia ni kuwakera tu ila kuhusu kuumwa siyo kweli ni juzi tu nimepima na nimeweka vipimo vyangu kwenye mitandao ya kijamii, mimi ni mzima jamani wa afya njema.
SWAGGAZ: Kwahiyo sasa hivi una kilo ngapi na kipi kilisababisha upungue?
Wema: Nimefikisha kilo 65 na lengo langu lilikuwa nikuwa na kilo hizo, nimekuwa mwepesi kupita maelezo pia kuna kipindi nguo ambazo navaa ni madera tu ila kwasasa naweza kuvaa nguo yoyote nikapendeza na kuwa na mwonekano mzuri.
Kilichofanya nipundue ni dawa, nilitumia madawa mengi mpaka kuwa na mwili huu.
SWAGGAZ: Mwaka umeanza, mashabiki zako watarajie nini?
Wema:2020 ni mwaka wangu, nimejipanga kufanya vema kwenye tasnia, wakae mkao wa kula kwani Wema wasasa sio wa yule wa miaka ya nyuma.
SWAGGAZ: Asante kwa muda wako.
Wema: Nashukuru sana.