27.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Ajira zisiishie kwa madaktari tu

TUNAWEZA kusema kwa uhakika miongoni mwa kauli ambazo zimepokelewa kwa furaha katika sekta ya afya, ni ile ya Rais Dk. John Magufuli kutangaza kutoa ajira kwa madaktari 1000.

Rais Magufuli ambaye alitoa uamuzi huo juzi katika mkutano wake na Chama cha Madaktari nchini na watumishi wengine wa sekta ya afya mbali na kukiri kutambua uwepo wa madaktari 2700 ambao hawaja ajiriwa  alisema mbali na kuanza kuchukua polepole madaktari hao 1000 mambo yakiwa mazuri wataajiri wengine.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli katika sekta ya afya umekuja baada ya kauli nyingine nyingi zilizopata kutolewa huko nyuma kuhusu tatizo la ajira si tu katika eneo hilo bali na mengine. 

Wiki kadhaa zilizopita Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alielezea kwa takwimu jinsi changamoto ya ajira linavyoelemea sekta ya sheria.

Jaji Mkuu ambaye alikuwa akizungumza katika hafla ya kuwaapisha mawakili wapya 558 iliyofanyika jijini Dar es Salaam mapema mwaka huu alieleza jinsi hata taasisi za Umma ambazo awali zilikuwa zinaajiri asilimia kubwa ya wahitimu wa shahada ya sheria zilivyopunguza kasi ya kutoa ajira.

Jaji Mkuu si wa kwanza kuzungumzia ukubwa wa tatizo la ajira nchini, katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose’ (Maisha yangu, Kusudi  Langu), Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameelezea hofu ya kukua kwa tatizo hilo katika maeneo yote.

 “Ninatishika kwa kweli ninavyoona vijana wengi wakiwa mitaani bila ya kuwa na shughuli ya kufanya na kibaya zaidi hakuna mipango ya haraka ya kukabili tatizo lao la ajira,” anasema Mkapa.

Katika kitabu chake hicho Mkapa ameshauri nchi ije na mipango endelevu kukabili tatizo la ajira kwa vijana na hasa wale wanaohitimu vyuo na shule mbalimbali.

Mkapa anasema aligundua ukubwa wa tatizo hilo katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuonya kuwa litakuwa ajenda kubwa ya mustakabali wa taifa katika chaguzi zijazo kutokana na ongezeko la idadi ya vijana.

Mbali na Mkapa mwingine ambaye alionya juu ya tatizo hilo hivi karibuni ni Waziri  Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya ambaye alisema suala hilo linahitaji kuangaliwa vyema ili kuwanusuru vijana ambao kwa sasa wengi wao wanashindwa kuwa wazalishaji katika mfumo rasmi.

Alisisitiza tatizo la ajira linazidi kukua kutokana na ongezeko la watu.

Alishauri tatizo hilo linahitaji kukabiliwa kwa kuangalia vyanzo vyote muhimu vinavyoweza kuzalisha ajira.

Mara kadhaa huko nyuma Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa naye amepata kuonya kuhusu tatizo la ajira na hata wakati fulani kujikuta akingia katika mvutano na Serikali ya awamu ya nne.

Wakati huo aliyekuwa Rais wake, Jakaya Kikwete alijitokeza hadharani kumjibu pasipo kumtaja jina akiwataka wanasiasa wanaozungumzia suala hilo kupendekeza suluhisho badala ya kuhubiri tatizo.

Lakini pamoja na hayo yote takwimu alizozitoa Jaji Mkuu kwenye eneo la sheria ni kama zimewasha taa nyekundu.

Alisema takwimu kutoka Sekretarieti ya Ajira na Utumishi wa Umma zinaonesha idadi ndogo ya wahitimu wa sheria walioomba kujaza nafasi za kazi ndio walifanikiwa kupata ajira. 

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu mwaka 2011/2012 walioomba walikuwa 157, waliopata 10 sawa na asilimia 6.3, mwaka  2012/2013 walioomba 306, waliopata 186 sawa na wasilimia 60 mwaka 2013/2014 walioomba 352, waliopata 24 sawa na asilimia 6.8.

Aliongeza kuwa mwaka 2014/2015 walioomba 186, waliopata 76 sawa na asilimia 40 na mwaka 2015/2016 walioomba 160, waliopata 38 sawa na asilimia 23.7 na mwaka 2016/2017 walioomba walikuwa 0, waliopata walikuwa 0.

“Kwa mwaka 2017/2018 walioomba 3250, waliopata 88 sawa na asilimia 2.7 na mwaka 2018/2019 walioomba 2826, waliopata 19 sawa na asilimia 0.6,” alisema Jaji Juma.

Pamoja na kwamba changamoto ya ajira ni ya kidunia na ushauri wa wengi ni kuwataka vijana wajiajiri, watumie utalaamu wao kibiashara na kutafuta fursa maeneo mengine lakini sisi tunaamini suala la ujenzi wa ajira kwa kiasi kikubwa linategemea Serikali.

Serikali ni rahisi kuwezesha upatikanaji wa ajira kupitia mfumo wa ajira za serikali, na zaidi ushiriki wake katika kuziwezesha sekta binafsi ambazo nazo ni mwajiri mwingine mkubwa.

Pamoja na hayo ni ukweli usiopingika licha ya wengi kujua fursa zinazowazunguka na jinsi ya kuzitumia, bado suala la mtaji, mazingira na kodi zinazobuniwa mara kwa mara hususani Halmashauri, Manispaa na vijiji limebaki kuwa tatizo kubwa.

Ipo mifano ya vijana ambao wameungana kujaribu kupambana na tatizo la ajira lakini wengi wao wamejikuta bado katika mazingira magumu kutokana na taratibu ngumu wanazokutana nazo ama kwenye taasisi za kifedha, TRA, Halmashauri nk.

Tunaamini Serikali inayo mikakati na mapendekezo mengi ya kukabiliana na tatizo la ajira, lakini tunashauri  alichoanza kufanya Rais Magufuli katika sekta ya afya kiendelee pia kwenye kada nyingine.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,554FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles