Na Samwel Mwanga, Bariadi
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama amepiga marufuku kualikwa katika makongamano, semina na warsha   kujadili changamoto zinazowakabili vijana.
Alitoa kauli hiyo jana wilayani Maswa   wakati akizindua kikundi cha Vijana cha Maswa Family Enterprises.
Mhagama alisema kwa sasa atakuwa anaalikwa kuona na kufungua miradi na viwanda vya vijana na vya kina mama wajasiriamali ili kuwaondoa katika kundi la kuwa wategemezi.
‘’Kuanzia leo kiongozi yeyote wa nchi hii asinialike kwenye kongamano, warsha au semina nitakuwa naalikwa kufanya kazi kama hii leo ya kufungua viwanda na miradi mingine,’’ alisisitiza.
Alisema   serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na vijana wenye lengo la kujiletea maendeleo kwa kuanzisha viwanda vidogo kupitia umoja wao.
Vijana wa kikundi cha kuzalisha chaki wameonyesha njia kwa vijana wa Tanzania na wamefanya kumbukizi katika wiki la vijana na maadhimisho ya kifo cha Mwalimu  Nyerere, alisema.
Alisema hataki kazi hiyo iingiliwe na vyama vya siasa, timu ipo ya mkoa kwa ajili ya vijana wanyonge na siasa zisiharibu viongozi wa mkoa.
Waziri alisema pia kuwa atawasiliana na Wizara ya Viwanda kuona uwezekano wa serikali kupiga marukufu kuagiza chaki nje ya nchi kwa kuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika viwanda kama hivyo.
Awali Mwenyekiti wa kikundi hicho, Kelvin Steven alisema lengo la kikundi  ni kufanya shughuli za  jamii na uzalishaji mali..
Alisema mahitaji ya chaki Mkoa wa Simiyu ni katoni 667 kwa mwezi na  wao watakuwa na ziada ya katoni 1883 ambazo watauza nje ya mkoa.
Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo alisema vijana wakiwezeshwa hasa katika kuanzisha viwanda vidogo watapunguza umaskini na utegemezi.