Na ELIYA MBONEA-ARUSHA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, amewaomba radhi akina mama kwa kutozingatia uwiano wa uteuzi wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA).
Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa alipokuwa akizindua rasmi shughuli za bodi hiyo mpya iliyoteulewa hivi karibuni ikiwa na wajumbe wanaume 11 na mwanamke mmoja, hivyo kukamilisha idadi ya wajumbe 12.
Akizungumza na wajumbe wa bodi hiyo na Menejimenti ya NCAA, Dk. Kigwangalla, alisema katika uteuzi huo alihakikisha anazingatia vigezo zaidi kutoka kwa wajumbe.
“Najisikia aibu kwa sababu sikuweka mizania sawa, nakiri siku-balance, akina mama naomba mnisamehe. Wakati ujao tutazingatia vigezo ambavyo watu wa nje waliviona.
“Nakiri kukosea, hata baada ya kuwatangaza nisingeweza tena kuivunja bodi. Hivyo ngoja twende na bodi hii kwanza japokuwa humu ndani pia yupo mwanamke,” alisema Dk. Kigwangalla.
Bodi hiyo inayoongozwa Mwenyekiti Professa Abiud Kaswamila, ina mjumbe mwanamke mmoja, Professa Kaunde Sibuga kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Morogoro (SUA).
Akizungumzia uteuzi huo kwa upande wake, Prof. Sibuga alisema kwa kawaida wajumbe wa bodi huteuliwa na waziri mwenyewe kwa kutumia vigezo na sifa anazozijua yeye.
“Kwa kweli hata mimi naweza kusema baada ya kuangalia orodha ya majina ya wajumbe nilishtuka kujiona niko peke yangu.
“Lakini ukweli ni kwamba ukiwa kwenye bodi au kikundi chochote kilichopewa majukumu, cha msingi ni kufuata taratibu zilizopo kufanya kazi na kushirikiana na wajumbe na mejimenti iliyopo.,” alisema.
Profesa Sibuga, alisema kwanza anayo faraja kubwa ya kuwa mwanamke kwenye bodi, huku akiahidi kutoa mawazo makini kwenye nafasi yake.
Wajumbe wengine ni Brigedia Jenerali mstaafu Aloyce Mwanjile, Bakari Nampenya, Deogratius Pisa, Edward Nduleti, Freddy Manongi, Haruna Masebu, Humphrey Mniaichi, Jumanne Feruzi, Michael Kamazima, Mhandisi Peter Ulanga na Ruzika Mheto.