29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

CCM, CHADEMA, CUF WATAMBIANA KINONDONI, SIHA

Na WAANDISHI WETU-DAR/SIHA


TAMBO za uchaguzi wa marudio wa ubunge katika majimbo ya Kinondoni na Siha zimepamba moto, huku vijembe vikitawala kwa wagombea wa vyama hivyo.

Kufanyika kwa uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Februari 17, mwaka huu  kumetokana na kujiuzulu kwa wabunge wa majimbo hayo.

Akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana Mtambani Kata ya Mzimuni Dar es Salaam wakati wa kumnadi mgombea wa Chadema, Salum Mwalimu, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema uchaguzi huo ndio utakaotoa tathimini ya malengo yao ya kuua upinzani kama wamefanikiwa au laa.

Alisema ndani ya miaka miwili waliyofanyakazi na mgombea wa CCM, Maulid Mtulia wakati huo akiwa CUF wamebaini alikuwa ni mzigo wa misumari.

“Hii ni fursa kwetu tuliopewa na Mungu ya kumpata mbunge anayefaa tofauti na yule msaliti aliyekuwa mzigo,” alisema Mbowe.

Kwa upande wake mgombea ubunge wa Chadema, Salum Mwalimu aliwaomba wananchi wa Kinondoni wamchague ili atatue kero zao kwa kuwa ni mtu makini na akamtaka Mtulia kumfuata ili akampe namba za viongozi wa dunia nzima kama anaona ni suluhisho.

Azzan aibuka

Naye aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni kupitia CCM, Idd Azan ameibuka na kusema kuwa alikuwa anapiga simu kwa Rais wa Awamu ya Nne,  Jakaya Kikwete kuzuia bomoa bomoa kwa wakazi wa eneo la Hananasif,  Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni wa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo katika Kata ya Hananasifu, Azan alisema kila aliposikia kuwa tingatinga linakuja kuvunja nyumba aliongea na Rais na kuzuia.

Alisema haikuwa rahisi kwa Maulid Mtulia kuweza kufanya hivyo kwa kuwa alikuwa upande wa upinzani.

“Asingeweza kupiga simu kwa rais kwa kuwa alikuwa amejenga ukuta badala ya daraja ndio sababu alikimbilia kuzuia mahakamani,” alisema Azan.

Kwa upande wake, Mtulia alisema alipokuwa Chama cha Wananchi (CUF) hakuruhusiwa kuwa na namba ya Rais lakini kwa sasa anayo hivyo hata likitokea tatizo usiku atapiga simu kwa Rais.

“Kwa sasa ninakwenda kupeleka kilio cha bomoabomoa kwani sina uwezo wa kuwajengea nyumba wala kuwapa viwanja waliobomolewa,” alisema Mtulia.

CUF NA AHADI

Naye mgombea ubunge wa CUF, Rajab Salim, alisema anaomba ubunge ili aweze kuwatumikia wananchi wa Kinondoni kwani awali walipata mwakilishi ambaye amewasaliti kwa masilahi yake binafsi.

Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika kwa Manyanya, alisema amejipanga kuhakikisha anashughulikia kero za wanakinondoni kwa vitendo ikiwemo kuhakikisha anakwenda bungeni kusimamia suala la maji, afya na elimu.

“Nimejipanga kuwatumikia ninawaomba Februari 17, mniamini kwa kunichagua kwa kura zote ili niwatumikie. Nimjipanga kufanyakazi mtakayonituma kwa vitendo na si maneno ua kuwasaliti kama walivyofanya wengine,” alisema Rajab

CCM SIHA

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa,Humphrey Polepole amewaahidi wananchi wa Kijiji cha Magadini Kata Gararagua kumegewa eneo zaidi ya ekari 3500 kwa ajili ya wafugaji katika mashamba ya NARCO.

Polepole aliyasema hayo kwenye mkutano wa kumnadi mgombea ubunge jimbo la Siha Dk. Godwin Mollel kupitia CCM .

Alisema kuwa baada ya uchaguzi  CCM itailekeza serikali kuwapa wafugaji waishio katika kata hiyo ekari zaidi ya 3500 kwa ajili ya ufugaji.

Mbali na hayo pia aliahidi kumalizia ujenzi wa Zahanati ya Magadini iliyopo Kata ya Gararagua.

 

Habari hii imendaliwa na Christina Gauluhanga, Tunu Nassor (Dar),  SAFINA SARWATT na OMAR MLEKWA (SIHA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles