Safina Sarwatt, Mwanga
Wawekezaji ambao wamepewa ardhi na wananchi wa vijiji vya Kivisini na Jipe, kwa ajili ya kuwekeza wametakiwa kuhakikisha wanatimiza masharti ya mikataba hiyo kwa haraka.
Hayo yabainishwa leo Februari 18, na Mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo, kwenye mkutano na wananchi wa kijiji cha Jipe wilaya ya Mwanga mkoani wa Kilimanjaro, uliokuwa na lengo la kuwashukuru pamoja na kupokea kero za wapiga kura waliompa ushindi wa kishindo mwanasiasa huyo.
Amesema kutokana na uwepo wa migogoro ya ardhi katika vijiji na kata wilayani humo, wenyeviti wa maeneo hayo wamewataka kupeleka muhtasari ya vikao waliyokaa baina ya wawekezaji hao na wananchi wa maeneo hayo ili kufikia mwafaka wa migogoro ya ardhi iliyoko katika maeneo hayo.
Tadayo amesema wenyeviti wa vijiji na kata wamekuwa wa kwanza kusababisha migogoro ya ardhi kutokana na tamaa binafsi badala ya kujali maslahi ya wanaowaongoza hivyo kuibua mgongano wa kimaslahi wa pande mbili.
Tadayo amewataka wawekezaji hao wafuate masharti ya mikataba yao ili kuondoa mgongano wa kimaslahi ambao umekuwa ukisababisha kuwepo migogoro mingi ya ardhi.
“Kama aliahidi kuwapatia ardhi ili awajengee zahanati, mradi wa maji au shule ahakikishe anatimiza ahadi hiyo na anapojenga ahakikishe anawashiriki wataalamu wa halmashauri ili asije kujenga chini ya kiwango baada ya mwaka mmoja mradi huo unakufa,” alisisitiza Tadayo.
Kwa upande wake Diwani wa Jipe, Dk. Ally Masoud Kidaya, amesema kuanzia Machi Mosi, mwaka huu, atakuwa na ziara ya kupitia kwenye vijiji kwa ajili ya kuzitatua changamoto hizo kwa haki na kuondoa dhuluma zinazoendelea katika eneo lake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa Kambi ya Simba, Siraji Msuya na Zainabu Mohamed, wamesema kumekuwa na ahadi zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa Maabara na wananchi wamekuwa wakijitolea kwa hali na mali lakini cha kushangaza viongozi wa kijiji na kata wamekuwa wakiwaangusha.
“Sisi wakazi wa Kambi ya Simba tulikuwa na eneo letu la ardhi ambalo tulilitoa kwa ajili ya ujenzi wa maabara, na tulichangishwa kila mmoja Sh 17,000 tulipeleka mchanga, na mawe lakini cha kushangaza hakuna ujenzi uliofanyika sasa ni mwaka wa tano na eneo hilo tayari limeshauzwa kwa mtu binafsi ambaye kwa sasa anaendeleza ujenzi wake,” amesema mkazi huyo.