Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
WATUHUMIWA katika kesi 13 zinazohusisha nyara za serikali zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 800 zilizokamatwa ndani na nje ya nchi wametoroka na kusababisha kesi kukwama.
Watuhumiwa hao waliua tembo 300, chui wanane, kobe 210, twiga, kiboko, pundamilia na ndege wa aina mbalimbali na iwapo wangehukumiwa kulipa faini wangelipa zaidi ya Sh bilioni tano.
Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa mwongozo kwa wapelelezi na waendesha mashitaka wa kesi za wanyamapori na misitu, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga, alisema watuhumiwa hao walitoroka baada ya kupewa dhamana.
“Mahakama inapotoa dhamana moja ya masharti yatolewayo ni washtakiwa kunyang’anywa hati zao za kusafiria lakini hili bado halijasaidia kuwazuia kutoroka,” alisema Mganga.
Alisema utafiti huo ulifanyika katika Mahakama za Mkoa wa Dar es Salaam kati ya mwaka 2010 hadi 2015, ambao kitakwimu una kesi chache za wanyamapori kulinganisha na mikoa mingine.
Alisema kati ya watuhumiwa hao asilimia 69 walikuwa ni raia wa kigeni na asilimia 31 walikuwa Watanzania.
“Hali hii ilinilazimu kutumia mamlaka yangu kisheria kuweka cheti cha kuzuia dhamana kwa washtakiwa wakubwa katika kesi zinazohusu meno ya tembo na vifaru ambao wanakaribia kutoweka nchini,” alisema.
Kuhusu mwongozo huo, alisema unaweka viwango na utaratibu utakaopaswa kufuatwa katika hatua zote za upelelezi na uendeshaji mashitaka kwa lengo la kuhakikisha kwamba kesi zinapelelezwa na kuendeshwa vizuri.
Alisema mwongozo huo unatarajiwa kuanza kutumika Januari mwakani ili kutoa mwanya kwa wapelelezi na waendesha mashitaka kupewa mafunzo juu ya matumizi na nyenzo mbalimbali zilizomo ndani ya mwongozo.
Kwa mujibu wa Mganga, mwongozo huo utajikita katika kesi zote zinazohusu tembo, kifaru, twiga, simba na mijusi ambayo hupatikana nchini pekee. Pia utahusisha kesi zinazohusu miti ya mpingo, mninga, sandarusi, mvule, mkoko na mingine.
Awali akifungua mkutano huo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliitaka Mahakama kuweka miongozo katika maeneo ya dhamana na adhabu ili kuwe na uwiano wa amri zitolewazo na majaji na mahakimu.