NA GUSTAPHU HAULE, PWANI
WATU 348 wamefariki dunia na wengine 1,039 kujeruhiwa katika matukio mbalimbali ya ajali yaliyotokea mkoani Pwani katika kipindi cha Januari 2015 na Septemba 2016 mwaka huu.
Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Pwani Abdi Issango, alitoa takwimu hizo juzi katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama yaliofanyika wilayani Chalinze.
Issango alisema katika kipindi cha Januari na Septemba 2015 jumla ya ajali 382 zilitokea ambapo kati ya hizo ajali za vifo zilikuwa ni 138, ajali za majeruhi ni 244 huku watu waliokufa ni 183 na majeruhi 637.
“Mwaka 2016 ajali zilizotokea ni 376 ikiwa ni pungufu ya asilimia sita lakini ajali za vifo viliongezeka na kufikia 148 sawa na asilimia 10 wakati ajali za majeruhi ni 228 huku watu waliokufa ni 165 na jumla ya majeruhi ni 402.
“Tathmini inaonyesha kuwa ajali hizo husababishwa na makosa ya kibinadamu ikiwamo madereva kuendesha mwendokasi, ulevi, uzembe wa watembea kwa miguu, ku-overtake sehemu zisizoruhusiwa na uelewa mdogo wa usalama barabarani kwa waendesha bodaboda,” alisema Issango.
Issango alisema kwa upande wa makosa yaliyokamatwa mwaka 2015 yalikuwa 560,65 na kusababisha makusanyo ya fedha kiasi cha Sh bilioni 1.6 huku mwaka 2016 yakiwa makosa 79,041 sawa na ongezeko la asilimia 40.98 na kufanya makusanyo kufikia bilioni 2.3.
Kwa upande wake kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ACP Boniventura Mushongi, alisema changamoto kubwa zinazokabili Mkoa wa Pwani ni pamoja na ufinyu wa barabara ya Dar es Salaam na Chalinze na ukosefu wa magari ya kuvuta magari baada ya ajali.
“Changamoto nyingine ni kukosekana kwa huduma ya zimamoto, ubutu wa sheria ya usalama barabarani, rushwa, ukosefu wa vitendea kazi, watendaji kutotimiza wajibu wao na mahakimu kushindwa kutoa adhabu zisizoendana na sheria ya usalama barabarani,” alisema.