Gabriel Mushi, Dodoma
Serikali imeagiza wakuu wa mikoa, wilaya na maofisa biashara kufuatilia na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wanaopandisha bei ya sukari kwa makusudi katika kipindi hiki cha kuelekea mwezi wa mfungo wa Ramadhani.
Pia imetoa vibali kwa wafanyabiashara kuingiza sukari nchini ili kukubaliana na mfumuko wa bei ya sukari nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa wakati akijibu swali la Mbunge wa kuteuliwa, Abdallah Bulembo ambaye alitaka kujua msimamo wa serikali kuhusu mfumuko wa bei ya sukari ambayo sasa umefikia Sh 3,200.
Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema tayari serikali imelitafutia ufumbuzi kwa kulenga kuhakikisha upatikanaji wa sukari uwe wa kutosha na kila mwenye mahitaji ya matumikzi aweze kupata bidhaa hii ikiwa wanaoanza mfungo,
“Ili kuweza kufanya soko la sukari kuendelea kuwepo na kupunguza bei ya sukari ya ndani, vibali tumeashaviagiza na tayari sukari imeanza kuingia na bodi ya sukari kupitia wizara ya kilimo inaendelea kufuatilia mwenendo wa uingiaji wa sukari nchini ili iweze kuifikia hadi ngazi ya vijiji na huduma ipatikane maeneo yote.
“Niwaondolee mashaka Watanzania hasa waislamu kwamba sukari itapatikana kipindi chote cha Ramadhani na maeneo yote ambayo yanahitaji sukari kupitia vibali tulivyotoa tutaendelea kufuatilia mwenendo wa bei ili watu wasipandishe kwa makusudi, tutafanya ufuatiliaji kwenye maduka kwani wakipandisha kwa makusudi watakuwa wanawaadhibu waislamu kwa sababu ya kuwa na mahitaji makubwa,” amesema.