24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wasomi wamchambua Majaliwa

kassim-majaliwaNa Tobias Nsungwe, Dar es Salaam

WAKATI Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, leo anatimiza mwaka mmoja tangu aapishwe, baadhi ya wasomi wamesema kasi na mwenendo wa utawala wa Rais Dk. John Magufuli, umefifisha utendaji wa majukumu ya kazi zake.

Majaliwa anatimiza mwaka mmoja huku nchi ikiwa inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo uhaba wa dawa hospitalini na watumishi hewa.

Majaliwa ametimiza mwaka mmoja tangu alipoteuliwa na Magufuli Novemba 19, mwaka jana na aliapishwa siku iliyofuata katika viwanja vya Ikulu Ndogo iliyopo Chamwino, Dodoma.

Wakizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa nyakati tofauti wiki hii, wasomi hao walisema mwenendo wa Serikali ya Magufuli umemfanya Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruhangwa, ashindwe kutimiza majukumu yake ya kushauri na kusimamia utendaji serikalini na hivyo kugeuka kuwa waziri mkuu anayeagizwa zaidi kuliko kuagiza.

Wasomi hao wamemwelezea Majaliwa kama mtu msikivu ambaye amekuwa na historia ya uchapakazi tangu akiwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) akishughulikia elimu na ndiko alikopata uzoefu, lakini kitendo cha Desemba, mwaka jana kuagiza wagombea walioshindwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana wasifanye mikutano ya siasa kulionyesha jinsi alivyoshindwa kumshauri Magufuli kwa sababu kukataza mikutano hiyo ni kuvunja Katiba ya nchi.

“Ni kumwonea Majaliwa kama mtu binafsi kwa kumfanyia tathimini peke yake kwa sababu nchi hii ina Executive President (Rais Mtendaji), hivyo mambo yote anayafanya kwa niaba na kwa mapenzi ya rais aliyemteua. Kwa hali hiyo sitakuwa na maoni kwa hili,” alisema Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Bashiru Ally.

Alisema Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 na ile ya Jamhuri ya mwaka 1962 zinampa rais madaraka makubwa na kwa aina ya utendajji wa Magufuli ni vigumu kumpambanua Majaliwa peke yake. “Waziri Mkuu hatarajiwi kumfunika rais. Tuliona huko nyuma mawaziri wakuu waliojaribu kutaka kumzidi rais na wakaipatapata,” alisema Dk. Bashiru.

Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Tumaini (Bukoba), Dk. Azaveli Lwaitama, aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa kitendo cha Magufuli kuipeleka Tamisemi Ikulu kutokana na kile alichokisema kuwa kumesababishwa na uozo uliojaa katika halmashauri, kinamfanya Majaliwa kuonekana kuwa na hadhi ya Mkuu wa Mkoa.

“Waziri Mkuu wa sasa amepunguzwa nguvu. Kwa kawaida yeye ndiye kiongozi wa Serikali bungeni na Tamisemi. Sasa kumwondolea Tamisemi kunamfanya Majaliwa kuwa na hadhi ya mkuu wa mkoa kwa sababu watu wengi waliopaswa wawajibike kwake sasa wanapokea maelekezo moja kwa moja toka kwa rais,” alisema Dk. Lwaitama ambaye pia aliwahi kuwa Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM.

Alisema kwa maoni yake Bunge limeng’olewa meno kiasi cha Majaliwa kuambiwa cha kujibu na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, wakati Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alipomuuliza swali katika Bunge la Novemba, mwaka huu kuhusu madai ya wabunge wa CCM kuhongwa na Serikali Sh milioni 10.

“Nasema tena kutathmini utendaji wake pekee ni kumwonea. Kwa aina ya rais proactive kama Magufuli anayefanya kazi nyingi za utendaji, kumemfanya Majaliwa kuwa mtendaji wa kutumwa, ndiyo maana tumeona akienda bandarini, hizi zote ni kazi za kutumwa na rais wake,” alisema Dk. Lwaitama.

Msomi huyo alisema kwa kawaida Majaliwa ndiye aliyepaswa kusimamia mambo yote ya Tanzania Bara, lakini inaonekana Magufuli ametoa uhuru zaidi kwa Serikali ya Zanzibar na kazi za huku kwetu anazifanya yeye. “Sasa hapo waziri mkuu ana kazi gani,” alihoji Dk. Lwaitama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles