30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yaendesha operesheni usiku wa manane

traNa Waandishi Wetu-DAR ES SALAAM

WAKATI kukiwa na taarifa kuwa Serikali imeshindwa kutekeleza bajeti yake ya mwaka 2016/17 kutokana na upungufu wa Sh bilioni 427, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanzisha msako dhidi ya wakwepa kodi hadi usiku wa manane.

Taarifa ambazo zimethibitishwa na maofisa wa mamlaka hiyo, zinasema kuwa TRA ikisaidiwa na Jeshi la Polisi, imeanzisha msako huo kuwasaka watu walioingiza na wanaoendelea kuingiza magari pasipo kufuata utaratibu, ikiwamo kutolipa kodi.

MTANZANIA Jumapili katika uchunguzi wake limebaini kuwa msako huu wa sasa ni tofauti na ule uliozoeleka wa kuyakamata magari yaliyokiuka taratibu nyakati za mchana, tena barabarani.

Uchunguzi huo umebaini kuwa msako huo unafanywa usiku, hususani katika majumba ya starehe ambayo watu wanakwenda kwa manunuzi, muziki au kuangalia sinema nk., hoteli, na maeneo ya katikati ya mji au jiji.

Hatua hii ya TRA, imekuja wakati Ripoti ya Benki Kuu (BoT) kuhusu mwenendo wa uchumi ikionyesha Serikali imeshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato ya mwezi Septemba kwa asilimia 16 tofauti na makadirio yaliyowekwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya BoT iliyotolewa mwezi uliopita, kutokana na mwenendo huo, huku wahisani nao wakichangia kiwango kidogo tofauti na matarajio kinachofikia Sh bilioni 400.9,  Serikali imelazimika kutoa Sh bilioni 387 tu kwa ajili ya miradi ya maendeleo  tofauti na Sh bilioni 824 zilizopangwa  kutolewa mwezi Septemba.

Inaelezwa kuwa mapato yasiyotokana na kodi yaliyokusanywa ni Sh bilioni 82.2 tofauti na makadirio ambayo yalikuwa ni Sh bilioni 225.7 kwa kipindi hicho.

Makusanyo ya kodi ya mapato yalikuwa ni Sh bilioni 573. 6 yakiwa yameporomoka kwa kwa asilimia 10 ya matarajio.

Ripoti inaonyesha kuwa Serikali kuu ilikuwa imekusanya asilimia 84.3 ya Sh trilioni 1.3 zilizokadiriwa, huku Serikali za mitaa zikikusanya Sh bilioni 41.2 tofauti na makadirio ya Sh bilioni 55.5.

Kutokana na hayo, operesheni ya sasa inayofanywa na TRA usiku wa manane, pengine ni mkakati wa Serikali kuwa na mbinu mpya ya kuongeza mapato, hasa kutokana na upungufu huo uliojitokeza.

Mmoja wa waandishi wa MTANZANIA Jumapili aliwashuhudia maofisa wa TRA wakiendesha operesheni hiyo ya usiku katika majengo maarufu jijini Dar es Salaam yajulikanayo kama Dar Free Market.

Maofisa hao wa TRA wakiwa wamepewa ulinzi wa polisi waliovalia sare za operesheni, walifika eneo hilo saa 6:00 usiku wakiwa na gari la Serikali na kufanikiwa kumkamara mtu mmoja mwenye asili ya India, ambaye alikuwa akitaka kuondoka na gari lake aina ya Land Cruiser.

Mwandishi wa MTANZANIA Jumapili ambaye alifuatilia kwa ukaribu mazungumzo yao, alisikia maofisa hao wakijitambulisha kuwa wanatoka katika Kitengo cha Forodha, TRA.

Katika mazungumzo hayo, mtu huyo alilazimika kuwaita ndugu zake watano na muda mfupi baadae alifika mama mmoja ambaye alionekana akionyesha kitambulisho, huku akisikika akisema gari hilo lina msamaha wa kodi.

Hadi mwandishi wa MTANZANIA Jumapili anaondoka katika eneo hilo saa 7:30 usiku, ofisa huyo wa TRA, polisi na mtu huyo bado walikuwa wakiendelea kuvutana.

Mbali na gari hilo, polisi alionekana kulinyooshea gari jingine ambalo lilikuwa limeegeshwa katika eneo hilo likiwa halina namba za usajili.

Taarifa zaidi zilizokusanywa na gazeti hili, zinaeleza kuwa TRA wameanza operesheni hiyo kwa takribani mwezi sasa na magari ambayo yamekuwa yakikamatwa ni pamoja na ‘teksi bubu’ ambazo mara nyingi hufanya kazi usiku huku zikiwa hazina vibali ikiwamo leseni ya barabarani (Road license).

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili  Dar es Salaam, Ofisa Kodi Mkuu wa TRA, Sydney Mkamba, alisema ukamataji wa magari hayo ni sehemu ya utendaji kazi wa TRA waliojiwekea, na kwamba lengo ni kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa kwa hiari.

Mkamba alitaja maeneo yaliyolengwa katika operesheni hiyo kuwa ni wale walioagiza magari kwa kutumia mgongo wa taasisi zilizosamehewa kodi au taasisi hizo kuyauza kwa watu binafsi.

“Kuna baadhi ya taasisi ambazo hupewa msamaha wa kodi pindi wanapoingiza magari nchini kwa matumizi kulingana na kazi zao, lakini baadaye huamua kuyauza kwa watu wasiokuwa na msamaha hali inayosababisha kodi ya Serikali kupotea,” alisema.

Alilitaja eneo jingine kuwa ni lile la baadhi ya watu wanaouziana magari kwa kutumia fursa ya vibali vinavyotolewa kwa magari ya nchi jirani yanayokuja kutumika kwa muda hapa nchini.

“Mbinu nyingine inayotumiwa kuingiza magari yasiyolipiwa kodi ni ile ya kutumia mipaka isiyo rasmi, hivyo na sisi kama mamlaka kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tunayafuatilia magari yote tunayoyashuku kuwa yamekwepa kodi na tunapobaini basi tunayakamata,| alisema.

Mkamba alisema inachofanya TRA kwa sasa ni kwamba kila mtu atalipia kodi kulingana na aina na thamani ya gari, na kama atakuwa amelinunua kutoka kwenye taasisi yenye msamaha, basi atapigiwa hesabu kulingana na uchakavu wake.

Alisema katika kuhakikisha wanaongeza mbinu ya ukamataji wa magari yanayokwepa kodi, TRA imekuwa ikiwapeleka maofisa wake katika Chuo cha Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro kupata mafunzo ya kiaskari pamoja na mbinu zote za upelelezi na uchunguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles