26 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

WASICHANA WENGI WANAKABILIWA NA ATHARI YA KUTOJITAMBUA – CDF

NA GABRIEL MUSHI


KUJITAMBUA ni hali ya kuwa na ufahamu au uelewa wa kutosha juu ya maisha yako pamoja na mazingira yanayokuzunguka na hivyo kukufanya uishi maisha yanayofanana au kulingana na kiwango cha ufahamu ulionao au kiwango cha kujitambua kwako kutegemeana na nguvu ya taarifa unazopata.

Pia unaweza kusema kuwa ni mojawapo ya somo ambalo halijapewa kipaumbele ndani ya jamii yetu licha ya kwamba humsaidia mtu kuelewa au kujitambua  yeye ni nani, anapaswa kufanya nini, kwa sababu ipi, lini na katika muktadha upi.

Asilimia kubwa ya waathirika wa athari ya kutojimbua ni wasichana ambao kwa namna moja au nyingine elimu hii ya kujitambua ni adimu kwao.

Kwa kuwa elimu hii hujikita ndani ya nafsi ya mtu na kumfanya kuonekana mwenye busara na hekima katika uongeaji, kiuamuzi na kimatendo, taasisi mbalimbali zimeanza kujikita katika kuwafundisha wasichana mbinu mbalimbali kuhusu elimu hii ya kujitambua ili kukabiliana na changamoto wanazokumbana nazo ndani ya jamii.

Mojawapo ya taasisi hizo ni Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) ambalo ni shirika la hiari lisilo la Kiserikali, lililojikita katika mikoa ya Dar es Salaam, Mara na Dodoma kwa lengo la kutekeleza program na mipango yenye kukuza, kutetea na kuboresha haki na ustawi wa mtoto wa Kitanzania.

Hivi majuzi, shirika hilo liliendesha mafunzo ya kujitambua kwa wasichana Kata ya Kitunda iliyopo jijini Dar es Salaam yaliyolenga kuwawezesha wasichana kujijengea uwezo wa kujitambua, kujiamini, kujieleza, kufanya maamuzi yalio sahihi ikiwemo kujipangia mipango binafsi ya maendeleo.

Ofisa programu kutoka CDF, Amina Ally, anasema shirika hilo kwa kushirikiana na ubalozi wa Sweden waliandaa mafunzo hayo yaliyoshirikisha jumla ya wasichana 17 wenye umri wa miaka kati ya 17-24 na walio nje ya mfumo wa shule,

Anasema CDF imelenga kuendeleza harakati za kulinda na kutetea haki za watoto  na kukuza usawa wa kijinsia, hususani kwa watoto wa kike na kuhakikisha wasichana wanajiamini na kupata nafasi ya kupanga maisha yao binafsi bila kupangiwa na mtu mwingne.

“Tunatambua kuwa si wasomi wote hapa duniani na Tanzania ikiwamo ambao hubahatika kuipata elimu ya kujitambua pamoja na kwamba husoma vitabu vingi na kupata vyeti lukuki, lakini bado hushindwa kupata elimu ya kijitambua. Ndio maana baadhi ya watu hutenda matendo ambayo hayaendani na unavyowaona na unavyowategemea wafanye.

“Kutokana na hali hiyo, tumeona ni muhimu wasichana hawa kujitambua ili waweze kujifahamu, pia kufahamu vitu muhimu kwao, baada ya hapo wanaweza kutambua nafasi yao kama wanawake na jamii inamtazamo gani kwao, ikiwemo vikwazo vya kijinsia wanavyopitia na mwishowe watafanikiwa kuja na njia itakayowawezesha kukabiliana na vikwazo vilivyopo,” anasema.

 

FAIDA YA KUJITAMBUA
Amina anasema iwapo msichana atajitambua, hali hiyo itamwezesha kwa kila akifanyacho kuelekeza au kulenga kuchochea na kuleta maendeleo katika jamii husika.
Pili kuwa jasiri au mwenye msimamo thabiti kwa analoamini ni sahihi bila kuyumbishwa na mtu yoyote. Pia  kufikia malengo chanya na hata kuwa kioo cha jamii kwa maana nyingine kuwa barua isomwayo na kila mtu.

 

MADHARA YA KUTOJITAMBUA
Pamoja na mambo mengine, Amina anasema madhara ya kutojitambua huathiri jamii moja kwa moja hasa ikizingatiwa wasichana au wanawake ndio wasimamizi wakuu wa familia.

“Kutojitambua huzorotesha maendeleo kwani mlengwa hufanya mambo ovyo), hii husababisha migogoro kuongezeka katika jamii. Mtu asiyejitambua huwa chanzo cha migogoro na kero kubwa katika jamii,” anasema.

Anasema wanawake ni nguzo lakini hazionekani licha ya kufanya kazi zinazoleta faida katika nchi.

 

KUJIWEKEA MALENGO

Katika mafunzo hayo, wasichana walifanikiwa kujitengenezea mpango binafsi wa maendeleo, kila mmoja aliweka malengo yake yatakayomuongoza.

Mmoja wa wasichana walioshiriki mafunzo hayo, Diana Albert, anasema juhudi za makusudi inabidi zichukuliwe kuwaokoa wanawake ili kuwawezesha kuwa wafanyabiashara, watafiti na hata washauri.

Mmoja wa washiriki wa semina hiyo, Josephine Marwa, anasema wanawake wanaweza, hivyo ni vyema wakajishughulisha ili kujiingizia kipato na kujiepusha na utafutaji wa fedha kwa njia ambazo zinawadhalilisha.

“Bahati mbaya wanawake wengi wameachwa kuwa wa kuchota maji, kupika, kufanya biashara za uchuuzi, kulima na sasa hivi kucheza vigodoro. Juhudi za hapa na pale zinafanywa kuwaendeleza kibiashara mfano kuwasisitiza kujiunga na vikundi lakini kama taifa tunaweza kunufaika na uwezo wao ambao ni wa kipekee,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles