HARARE, Zimbabwe
MASWALI yameibuka iwapo kiongozi wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe au mkewe Grace wamepanga kutumia chama kipya kuwania urais katika uchaguzi ujao.
Mjadala huo umezuka baada ya wanasiasa wakongwe ambao ni washirika wa karibu wa Grace, kuunda chama kipya cha New Patriotic Front (NPF).
Hata hivyo, binamu yake Mugabe, Patrick Zhuwao amekanusha madai hayo huku akisema kuwa kiongozi huyo mkongwe aliyeng’atuliwa madarakani Novemba, mwaka jana, hatawania urais tena.
Wanasiasa wakongwe wanaodaiwa kuunda chama hicho, wameishutumu Jumuiya ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU) kwa kushindwa kuyashutumu mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Serikali ya Mugabe, mwaka 2017.
“Si kweli kwamba Mugabe analenga kurejea tena katika siasa. Hatuwezi kumtwika tena mzigo wa kuongoza nchi, mzee anapumzika,” alisema Zhuwao bila kugusia kuhusu Grace.
Mugabe, 93, ambaye aliongoza nchi hiyo tangu 1980, aling’olewa mamlakani mwaka 2017 na jeshi la nchi hiyo katika kile kilichoonekana ni ‘kuzima’ ghafla ndoto ya mkewe Grace, kumrithi.