Na Mwandishi Wetu, ARUSHA
WANANCHI waishio katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru,wametakiwa kutunza mazingira ikiwamo kuzingatia upandaji miti katika vyanzo vya maji.
Kauli hiyo imetolewa jana na Ofisa Mazingira kutoka Halmashauri hiyo,Sai Manyanda,alipokuwa akizungumza katika zoezi la uhamasishaji miti katika vyanzo vya maji kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na masuala ya usawa wa kijinsia.
Amesema hivi sasa dunia inakumbwa na mabadiliko makubwa ya tabia nchi hivyo wananchi hawana budi kushirikiana na serikali na wadau wengine wa maendeleo katika kutunza mazingira ikiwamo kuacha kukata miti.
“Nipongeze waandaaji wa kampeni hii na niombe ikawe chachu ya kuamsha ari ya kila mwananchi katika kukabiliana na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuanza na upandaji miti.
“Tutunze mazingira na tusiharibu vyanzo vya maji, kufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo hivyo,”amesema.
Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shirika la Voice Of Youth Tanzania(Voyota),Vincent Uhega,ambao ndiyo waandaaji wa kampeni hiyo, amesema wameamua kufanya kampeni hiyo kwa kushirikisha vijana katika kipindi hiki dunia inakabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tumeamua kutumia vijana kama njia sahihi ya kupeleka ujumbe na kuhamasisha jamii juu ya utunzaji mazingira na tumejipanga kuendelea kupanda miti na kutoa elimu kwa jamii juu ya utunzaji wa mazingira,”amesema
Naye mratibu wa programu ya vijana katika Chuo cha MSTCDC,Catherine Mosi,amesema wao kupitia jukwaa la vijana wanahamasisha kundi hilo kuchukua hatua kwenye changamoto mbalimbali ikiwemo ya mabadiliko ya tabia nchi.
“Tunahamasisha vijana kuchukua hatua na tahadhari kwenye kusaidia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ili watunze mazingira na mwitikio tunauona ni mkubwa,” amesema.