Na GURIAN ADOLF- SUMBAWANGA
HOFU imewakumba baadhi ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Sekondari Kirando wilayani Nkasi mkoani Rukwa, baada ya kuanza kuugua ugonjwa usiojulikana.
Baadhi ya wanafunzi walionekana kupatwa na kwikwi, kushindwa kuongea, kutetemeka na kuishiwa nguvu ghafla.
Ugonjwa huo umekuwa ukiwapata wanafunzi wa kike ambao wanasoma kidato cha tano na sita katika shule hiyo na kusababisha hofu kwa wazazi wa watoto hao huku wengine wakitaka kuwatorosha shuleni hapo na kuwapeleka kwa waganga wa kienyeji wakiamini kuwa watoto wao wamerogwa.
MTANZANIA liliwasiliana na mkuu wa shule hiyo, Erneo Mgina ambaye alikiri kuwapo kwa ugonjwa huo ambapo alisema ugonjwa huo umekuwa ukitokea mara kwa mara.
Alisema baada ya kuibuka kwa ugonjwa huo wa ajabu, amekuwa akiwapeleka wanafunzi hao katika kituo cha afya cha Kirando kupata matibabu.
Mgina alisema baada ya kulazwa na kupatiwa matibabu, baadaye huruhusiwa kurudi shule kuendelea na masomo yao kama kawaida licha ya kuwa baada ya muda unaibuka tena kwa wanafunzi wengine.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kirando, Dk. Gabriel Majani, alisema baada ya kufanyiwa vipimo wanafunzi hao hawakubainika kuwa na ugonjwa wowote tishio bali wana matatizo ya kisaikolojia.
“Mpaka sasa kuna wanafunzi wanane ambao hali zao si nzuri sana lakini wanapatiwa matibabu na tayari nimeshatoa taarifa ngazi ya wilaya na jitihada za kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo zinaendelea,” alisema Dk. Majani.