*Ilikuwa wauze mganga wa kienyeji Sh mil 6
Na Walter Mguluchuma-Katavi.
WAKAZI wanne Tarafa ya Mamba Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi, wamehukumiwa kifungo cha maisha jela, baada ya kukutwa na hatia ya kutaka kumuua mtu mwenye ulemavu wa ngozi kwa kumkata mkono wake, kisha kuondoka nao kwa lengo la kwenda kuuza kwa mganga wa kienyeji Sh milioni 6.
Waliohukumiwa kifungo hicho jana, ni Alex Manyanza Maliganya , Galila Nkuba (Malago) na Shile Dalushi.
Hukumu hiyo, ilitolewa na Jaji Richard Mashauri wa Mahakama Kuu ya Kanda ya Sumbawanga katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Katavi, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi 12.
Upande wa mashtaka uliwakilishwa na wanasheria wawili wa Serikali, Simon Peres na Dickson Makoro na washtakiwa walitetewa na mawakili,Elis Kifunda na Patrick Mwakyusa .
Awali katika kesi hiyo, wandesha mashtaka na wanasheria wa Serikali walidai washtakiwa kwa pamoja walienda kosa hilo Mei 14,2015 katika Kijiji cha Kinganda saa 6 usiku .
Walidai siku ya tukio, watuhumiwa walikwenda nyumbani kwao na mtu mwenye ulemavu wa ngozi, Lime Luchoma ambaye alikuwa amelala chumbani.
Walipofika walipojaribu kumuua kwa kumkata mkono wake wa kulia,kisha kuondoka nao.
Walidai baada ya kuchukua mkono mzima waliondoka nao, kisha kuubanika kwenye moto ili iwe rahisi kwao kuusafirisha kwenda kwa mganga wa kienyeji aliyekuwa amewaagiza.
Katika utetezi wao,washtakiwa waliiomba mahakama iwaachie huru kwa sababu maelezo waliyotoa mbele ya mlinzi wa amani katika Mahakama ya Mwanzo ya Mpanda Mjini walikiri kufanya kitendo hicho kutokana na kupata mateso ya kupigwa na polisi .
Wakili wa washtakiwa wa kwanza na wa pili, Eliasi Kifunda aliomba mahakama imwachie huru washtakiwa kutokana na kuwa na familia kubwa inayomtegemea na tangu kipindi ambacho amekaa mahabusu miaka 4 sasa familia yake imekosa malezi .
Pia mshtakiwa huyo bado ni kijana mwenye umri wa (28),akipewa nafasi ya kusamehewa anaweza kujirekebisha .
Mshtakiwa wa pili, aliomba mahakama iangalie kutoa adhabu ambayo inaweza kuwa na nafuu kwake kutokana na yeye kuwa na mri wa (44) familia yake inahitaji malezi yake .
Kwa washtakiwa watatu na wanne,Galila Nkuba na Shile Dalushi, waliokuwa wakitetewa na wakili Patrick Mwakyusa ambaye kwa upande wa mshtakiwa watatu aliomba huruma ya jaji kwa kuwa mshtakiwa huyo ana watoto tisa wanaomtegemea.
Mshtakiwa wa nne, aliomba mahakama imwachie huru kwa kuwa ana umri bado mdodo wa (31) na mkewe amefariki wakati akiwa mahabusu na ameaacha watoto watatu na kosa hilo ni la kwanza kwake .
Peres aliiambia Mahakama baada ya utetezi huo, kuwa matukio ya ukataji wa viuongo vya watu wenye ulemavu wa ngozi ni ukatili ambao hauvumiliki duniani.
Alisema hali hiyo, inawafanya watu watu wenye ulemavu wa ngozi kutoishi kwa amani katika dunia hii waliopewa na Mungu.
Alisema wengi wao, wamelazimika kuwa wakimbizi kwenye makazi ya familia zao na kuishi kwenye maeneo tengefu.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Richald Mashauri aliiambia Mahakama kutokana na ushahidi uliopelekwa mahakamani na upande wa mashtaka pasipo mashaka yoyote yale imeona washtakiwa wanayo hatia .
Alisema ushahidi uliouwa ukitolewa na upande wa utetezi wakati wa kusikiliza kesi hiyo umekuwa ukitofautiana, hali ambayo haiwezi kuiifanya mahakama kushawishika na kuwaona washtakiwa hawana hatia. Pia wazee washauri wa Mahakama wote kwa pamoja walisema kwenye maoni yao washtakiwa walitaka kuua .
Washtakiwa wametiwa hatiani chini ya kifungu cha sheria 211(a) cha sheria ya adhabu sura namba 16 marekebisho ya mwaka 2002.
Katika kesi hiyo, mahakama ilimwachia huru mshtakiwa wa sita, Masunga Kashindye ambaye baada ya kuchiwa alitimua mbio na kuelekea kusikojulikana ambapo mshtakiwa wa tano, Maiko Samweli alifariki dunia wakati akiwa mahabusu.
Mwisho