MWANDISHI WETU-SONGWE
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela, amefanya ziara ya kushtukiza katika baadhi ya shule za msingi na sekondari na kisha kumwagiza Ofisa Elimu Mkoa kuwachukulia hatua za kinidhamu walimu wote ambao wanachelewa au kutohudhuria shuleni.
Mwangela alitoa agizo hilo jana baada ya kutembelea shule za sekondari za Myovizi na Simbega pamoja na Shule ya Msingi Iyula katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na kubaini utoro na uchelewaji wa walimu mara baada ya kukagua madaftari ya mahudhurio.
“Mahudhurio ya walimu sio mazuri, walimu hawafiki wote katika shule zao na wengine huchelewa sana, pia vitabu vya mahudhurio havijafungwa ifikapo saa moja na nusu na saa moja na dakika 45 kama inavyotakiwa ili kuwabana wachelewaji,” alisema Mwangela.
Alisema kuwa Ofisa Elimu Mkoa anapaswa kusimamia mahudhurio ya walimu kwakuwa msingi wa taifa unajengwa shuleni na msingi huo hautaimarika endapo walimu watakosa nidhamu katika kuwahi na kuhudhuria shuleni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Myovizi, Tabu Mtafya, alisema amekuwa akitoa onyo kwa walimu ambao wanachelewa, hivyo agizo la Mkuu wa Mkoa ataendelea kulitekeleza.
“Baada ya mkuu wetu wa mkoa kukagua kitabu cha mahudhurio, ameniagiza niendelee kusimamia mahudhurio ya walimu, nami nitawaita walimu wote wa shule yangu niwakumbushe juu ya kuwahi na kutimiza wajibu wao,” alisema Mtafya.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo alikiri kuwepo kwa mapungufu ya walimu kutohudhuria au kuchelewa shuleni, na hivyo wamejipanga kusimamia mahudhurio ya walimu na kuwachukulia hatua za kinidhamu walimu watoro na wachelewaji.