Vijana 20 wanashikiliwa na polisi Visiwani Zanzibar kwa kushiriki na kuhamasisha uhusiano na ndoa za jinsia moja (ushoga) kupitia taasisi yao.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayub Mohamed amesema leo kuwa, vijana hao walikamatwa Septemba 15, mwaka huu katika Hoteli ya Mason, wakiwa wanafundishwa uhalali wa kuendeleza ndoa za jinsia moja.
“Vijana hao wenye taasisi inayoitwa Rich Initiative Organisation, walikuwa wakiwaelekeza wahudhuriaji ambao baadhi yao waliitwa kuwa mashuhuda wa wazazi kuwa wasiwe na tatizo kuwaona vijana wenzao wakijihusisha na uhusiano wa jinsia moja.
“Baada ya kukamatwa waliwekwa ndani wakafanyiwa upekuzi katika ofisi za taasisi hiyo, tumeona mawasiliano yao na taasisi za nje ambazo zina uhusiano nao, tutalisimamia hili hadi tutakapohakikisha tunaling’oa kwa sababu sio utamaduni wetu kabisa,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, Mkuu huyo wa Mkoa amesema ikithibitika taasisi hiyo inajishughulisha na ushoga itafutiwa usajili.