BENJAMIN MASESE-MWANZA
SERIKALI imesema wanawake wa Kanda ya Ziwa wamekithiri kunywa dawa za kienyeji wanapokuwa wajawazito kwa kuzichanganya kwenye uji na chai kitendo kinachochangia vifo, kutokwa na damu nyingi wanapojifungua, mimba kuharibika au kujifungua watoto wenye ulemavu.
Pia imetaja sababu kuu tatu zinazosababisha watoto wachanga 25 kati ya vizazi hai 1,000 kufariki dunia ni kushindwa kupumua ikiwa ni sawa na asilimia 31, kuzaliwa chini ya uzito (njiti) asilimia 25 na maambukizo ya maradhi mbalimbali yakiwamo Ukimwi ikiwa ni asilimia 20.
Hayo yamebainishwa jana na Afisa Programu ya Uzazi Salama kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Martha Shakinyau jijini Mwanza katika semina kwa waganga wakuu wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Shakinyau alisema amekuwa akizunguka katika hospitali mbalimbali nchini kutoa elimu ya uzazi salama kwa mama lakini amekutana na vituko vingi katika mikoa ya kanda hiyo.
“Ni jambo la kushangaza unakuta mama amekuja kwenye watalaam wa afya kujifungua lakini muda wote utaona ndugu zao wanampa dawa za kienyeji.
“Nyingine wanachanganya kwenye uji na chai sasa kitendo kile ni hatari sana kwani madaktari wanakuwa wanatoa dawa za kitalaam huku kumbe mama kanyweshwa miti asili.
“Matokeo yake unakuta mjamzito anatokwa na damu nyingi na kufariki, mtoto naye akibahatika kupona unakuta naye ana kasoro.
“Nimeshuhudia katika hospitali fulani nikiwa getini ndugu wa mjamzito wakilalamika wamepeleka chupa ya chai yenya dawa na uji ambao haukuwa na dawa, sasa wauguzi walimpa uji badala ya chai.
“Kumbe walitaka mjamzito anywe chai ambayo ina dawa asili ambazo wanaziamini angejifungua salama, nikafuatilia huyo mgonjwa wodini nikakuta ana hali mbaya na muda mfupi akawa amefariki,” alisema.