Na Beatrice Kaiza, Mtanzania Digital
WAJASIRIAMALI kisiwani cha Pemba wameeleza sababu zinazofanya biashara zao kutofikia masoko ya sehemu mbalimbali hasa kisiwa cha Unguja ni kutokana na uhaba wa vyombo vya habari katika kisiwa hicho.
Akizungumza katika kongamano la ‘Tunachonga Barabara’, lililoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wakubwa ya The warrior Women Foundation, msanii wa kuchora hina, Fatma Khamis, amesema katika biashara yoyote lazima kuwepo na muongozo ambao utawapa mwanga ya biashara.
“Pemba kuna vitu vyote kama tulivyozoea kutoa vitu sehemu mbalimbali kama Dar es Salaam, hivyo kungekuwepo kwa vyombo vya habari vikasimama kidete kwa ajili ya kujulisha watu kuwa hata Pemba vitu vipo tuunge Mkono wajasiriamali wa kwetu ingesaidia mno,” amesema Fatma.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wajasiriamali Kisiwa cha Pemba, Mzee Nyuki amempongeza mkurugenzi wa taasisi hiyo Sabra Machano kwa kuona umuhimu wa kufikiwa na kupewa elimu ya jinsi gani wanatainua masoko yao na kukabili changamoto ndogo na kubwa katika biashara zao.
“Ni mara ya kwanza tamasha hili kufanyika kisiwa cha Pemba japo lilizinduliwa Unguja lakini tumepata fursa ya kusikilizwa kero zetu,changamoto na kujua kwa namna gani hatufiki tunapopataka.
“Hivyo kupitia kongamano hili litasaidia zaidi wajasiriamali kujitambua, kufanya kazi kwa bidii, kuboresha biashara zao kwani tayari ipo taasisi ambayo imehaidi itashirikiana nasi bega kwa bega kuhakikisha tunapata masoko ya kutambulisha bidhaa zetu na kuhakikisha biashara zetu zinaleta faida,” amesema.