25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

WAFUNZWA KUTUMIA SILAHA  KUMLINDA KIM JONG-UN DHIDI YA WAMAREKANI

WATOTO wa shule nchini Korea Kaskazini hulazimishwa kushiriki katika aina tofauti tofauti ya michezo ikiwamo matumizi ya silaha kali.
Wakati wakifunzwa kumlinda Kiongozi wa Taifa hilo dogo la kikomunisti, Kim Jong-un jeshi la watoto hao wachanga lilionekana likikimbia huko na kule likiwa limejihami na silaha bandia aina ya AK-47s na magrenada ya kurusha kwa mikono.
 
Watoto hao wadogo walilazimishwa kukabiliana na vikwazo mbalimbali wakibeba Kalashnikovs feki huku umati mkubwa ukishuhudia katika sherehe zilizofanyika kwenye jengo jipya mjini  Pyongyang hivi karibuni

Mmoja wapo Myong Hyon-Jong (10) anaeleza kuwa anataka kujiunga na jeshi wakati atakapokuwa mkubwa ili kumlinda ‘kiongozi mpendwa wa taifa hilo mheshimiwa’ Kim Jong-un kwa nguvu ya kijeshi.”
Aliendelea kueleza kwamba wanapaswa kujiandaa wenyewe kulinda nchi yao.

Mwalimu wake Ri Su-Ryon kisha akasema mafunzo yamelenga kuwapatia watoto moyo wa kizalendo wa kuilinda nchi yao wakati watakapokuwa wakubwa na kujiandaa kimwili na kiakili kuwashinda maadui wowote wale.


Mara atakapomaliza kozi anasema: “Narusha grenada la mkono nikiwa na imani siku moja nitamrushia rasmi na kumshinda adui yeyote atakayejaribu kupenya ndani ya mipaka ya nchi yetu”.


Shughuli hiyo ilikuwa kusherehekea Siku ya Muungano wa Watoto Korea –inayosimamiwa na taasisi ambayo watoto wote nchini Korea Kaskazini wanakuwa moja kwa moja wanachama.
Lengo lake ni kuwapumbaza akili watoto wawe na heshima na watiifu na waaminifu kwa mamlaka na kuwa tayari kupigania kwa ajili ya Korea Kaskazini.


Watoto huaminishwa mamlaka zao zikiongozwa na kiongozi wao mkuu Kim Jung-un zina upendo mkubwa kwao, hazilali zikifanya kila ziwezalo kuwalinda na kuilinda nchi yao.
Na kwamba Marekani na washirika wao wengine ni adui yao mkubwa, mnyonyaji, mwenye kiu ya damu, ambaye anaweza kuwashambulia wakati wowote. Propaganda hii inawafanya waichukie vilivyo Marekani na kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya kiongozi na taifa lao.


Mara nyingi watoto au hata watu wazima wanapokutana na Kim huonekana wakilia katika kile kinachoonekana kuwa wanaigiza au wamepumbazwa akili kuonesha kilio chao ni mapenzi makubwa walio nayo kwake huku wakimchukulia kama mungu mtu.


Korea Kaskazini iko katika tahadhari kubwa ya uwezekano wa kuvamiwa na Marekani wakati wowote. Ni hali inayowafanya wakazanie na program za nyuklia na makombora ya masafa marefu licha ya kuwekewa vikwazo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.


Tangu kuanza kwa mwaka jana, taifa hilo limefanya majaribio kadhaa ya nyuklia na masafa marefu yanayoilenga Marekani, licha ya kwamba Rais Donald Trump kusisitiza hilo halitotokea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles