Na RAMADHAN LIBENANGA, MOROGORO
WAFUGAJI mkoani Morogoro, wameendelea kugoma kuchinja ng’ombe ili kuishinikiza Serikali isitishe upigaji chapa mifugo yao.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana, wafugaji hao walisema wamelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na uamuzi huo wa Serikali.
Kiongozi wa kundi la wafugaji hao, Mfalme ole Kelei, alisema tamko la Serikali la kukataza mifugo isiyopigwa chapa isiuzwe mnadani, ni dalili za unyanyasaji ambao hawako tayari kuukubali.
“Inawezekana lengo la Serikali ni zuri, lakini walitakiwa kutuelimisha kwanza na si kutoa amri pasipo kutushirikisha wafugaji.
“Kwa hiyo, hatutakubali kuchinja mifugo yetu hadi hapo watakapokuja na kutuelewesha faida za chapa hizo na madhara ya kutopiga chapa,” alisema ole Kelei.
“Narudia tena, tunamwomba waziri mwenye dhamana ya mifugo aje atutolee ufafanuzi wa suala hilo, vinginevyo hatutabadili msimamo wetu,” alisema ole Kelei.
Mgomo wa wafugaji kukataa kuchinja ng’ombe ulianza wiki iliyopita, baada ya wafugaji hao kugoma kutekeleza agilo la Serikali la kupiga chapa mifugo yao.
Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara wanaouza nyama mjini hapa wameanza kupandisha bei ya bidhaa hiyo, jambo linalowaumiza watu wenye kipato kidogo.