Na Florence Sanawa, Mtwara
Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), kimewaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na India ili kuongeza fursa za kibiashara nchini.
Akizindua kongamano la wafanyabiashara wa nchini India na Tanzania mkoani Mtwara leo Jumapili Machi 4, Mkuu wa mkoa huo, Gellasius Byakanwa amesema wafanyabishara wanapaswa kuchangamkia fursa ya kufanya biashara nchini India.
Amesema mazao kama mchele na korosho ambayo hupatikana kwa wingi nchini yatawanufaisha wafanyabishara wengi hasa hasa baada ya India kufungua milango ya kibiashara nchini ambayo ni nafasi nzuri ikitumiwa ipasavyo inaweza kuwanufaisha na pia kutolewa punguzo kwa hati ya kusafiria (Passport).
“Unajua hili jambo la kuondoa ushuru na kupunguza tozo ya hati ya kusafiria inaweza kuwavuta wafanyabiashara wengi zaidi kwenda huko kuchangamkia fursa hiyo adhimu kwetu, tuichangamkie fursa hii,” amesema Byakanwa.
Balozi wa India nchini Tanzania, Sandeep Arya amesema nchi hiyo ni miongoni mwa wawekezaji wakuu nchini Tanzania katika soko la kiulimwengu ambalo lina ushindani mkubwa zaidi.
“Sisi tunao watalaamu na tuna uwezo mzuri katika vyombo vya moto hata mahitaji yetu kimaisha na hapa yanafanana tukishirikiana kwa mbinu za kitaaluma tunaweza kusonga mbele,” amesema.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Mwenyekiti TCCIA mkoani Mtwara, Swallah Swallah amesema kitendo cha wafanyabiashara kupata fursa hiyo ni nafasi kwao kujitambua kibiashara kwa kuwa bidhaa zipo za kutosha zinazozalishwa.